Sunday 11 October 2015

WATAKIWA KUZITUNZA SHAHADA ZA KURA







Na Anna Nkinda, Lindi
WAKAZI wa mkoa wa Lindi wametakiwa kuzitunza shahada zao za kupigia kura na kukataa kurubuniwa ili waziuze kwani, kadi hizo ndizo zitazowawezesha kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.
Wito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama, Salma Kikwete wakati akizungumza kwa nyakati tofauti katika majimbo ya Mtama na Ruangwa, waliohudhuria mikutano ya kampeni ya kuwanadi wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kupitia tiketi ya CCM.
Mama Salma, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi Mjini, alisema kadi ya mpiga kura ndiyo itakayomuwezesha mwananchi aliyejiandikisha kumchagua kiongozi anayemtaka siku ya uchaguzi ikifika.
“Ikitokea mtu anakuja kwako na kukwambia nitakupa mkopo wa sh. 30,000 au 50,000 nipe kadi yako ya kupigia kura, usikubali. Ukimpa tu utakuwa umepoteza haki yako ya msingi ya kupiga kura kwani hatakurudishia hadi uchaguzi utakapoisha,” alisisitiza Mama Kikwete.
Aliwasihi wanawake kutoogopa siku ya uchaguzi ikifika, bali wajitokeze kwa wingi kupigakura kwani kutakuwa na usalama wa kutosha, ulinzi utaimarishwa na uchaguzi utaenda vizuri kama ilivyopangwa.
Aliwaomba kutopoteza kura zao bali wafanye maamuzi sahihi na kuwachagua viongozi kutoka CCM, ambao wamewaletea na wataendelea kuwaletea maendeleo endelevu kwa kuwa chama hicho kina Ilani ya Uchaguzi inayoeleweka ambayo ni mkataba baina ya CCM na wananchi.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye, alisema ushindi kwa CCM uko wazi na kuwataka wananchi wa Mtama kutembea kifua mbele kwani, serikali imefanya mambo mengi, ikiwemo kuimarisha huduma za afya, elimu, barabara, umeme na maji.
“Changamoto iliyopo ni kutokuwa na daraja katika mto Lukuledi kwani wananchi wanne wamepoteza maisha wakati wakivuka kwenda kulima ng’ambo. Mkinichagua nitahakikisha linajengwa kwani kazi ya serikali ni kutengeneza mazingira mazuri ili wananchi wake waweze kujipatia riziki,” alisema.
 
Naye mgombea ubunge wa jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kumchagua tena kwa kipindi cha miaka mitano kwani,  kazi aliyoifanya wameiona na anataka afanye tena kazi kubwa zaidi.
“Hivi sasa katika  jimbo letu tuna  walimu wa kutosha, maji yapo, barabara zipo. Kwa mfano, barabara ya Mandawa – Milola haikuwa inapitika  kirahisi, lakini sasa inapitika. Minara ya mawasiliano ipo na bado inaendelea kujengwa katika maeneo ambayo hakuna, umeme nguzo zinaendelea kusambazwa, nawaomba tuzidi kushirikiana ili turekebishe mapungufu yaliyopo,” alisema.
Majaliwa, ambaye ni Naibu Waziri wa TAMISEMI, alisema wananchi wa eneo hilo  wanakabiliwa na upungufu wa chakula kutokana na kutopata mvua za kutosha kipindi cha kilimo kilichopita  na kumuomba Mama Kikwete aweze kuwasaidia ili wananchi hao wapate  msaada wa chakula.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mandawa, jumla ya wanachama 34 walihamia CCM, ambapo wanachama  22 walitoka CUF na 12 CHADEMA.

No comments:

Post a Comment