Na Hamis Shimye, Pemba
MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia
CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali yake inaendelea na jitihada za
kufikisha umeme katika baadhi ya maeneo katika Jimbo la Mtambwe, Kaskazini
Pemba.
Amesema yako baadhi ya maeneo ambayo
umeme bado haujafika, hivyo atahakikisha unafika katika maeneo yote jimboni
humo.
Akizungumza katika viwanja vya Shule
ya Makoongeni, Dk. Shein alisema pamoja na kufikisha umeme katika maeneo hayo,
pia atajenga barabara zenye hadhi ya kimataifa.
"Umeme ni lazima na
nitahakikisha unafika Mtambwe yote, lakini pia tegemeeni barabara zenye
hadhi ya miji mikuu kama vile Dar es Salaam, Nairobi na Kampala.
“Nilipotembelea kituo kimoja cha
karafuu mwaka 2011, niliahidi kujenga barabara inayokuja Mtambwe, lakini
nimeambiwa barabara ile haikujengwa ipasavyo," alisema.
Kuhusu zao la karafuu, aliwaambia
wakazi hao wa Mtambwe kuwa serikali italisimamia ingawa wenzao wa Chama cha
Wananchi (CUF) sera yao ilikuwa ni kulibinafsisha.
Naye Balozi Ali Karume alisema CCM
haitoi ahadi za uongo ndiyo maana Dk. Shein alipoahidi gharama za kujifungua ni
bure, limetekelezwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
"Wanawatisha CCM ikishinda
watachoma nyumba za CCM moto, wataanzia wapi, kwani wao wanalala nje?" Alihoji
Balozi Karume.
No comments:
Post a Comment