Sunday, 11 October 2015

SAMIA: TUTASHINDA UCHAGUZI MKUU KWA ASILIMIA 90




NA KHADIJA MUSSA, SHINYANGA
MGOMBEA mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan amesema Chama kitashinda kwa zaidi ya asilimia 90 katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Amesema hatua hiyo inatokana na namna ambavyo wananchi walivyokuwa na imani na CCM pamoja na wagombea wa nafasi mbalimbali, wakiongozwa na mgombea urais, Dk. John Magufuli.
Kufuatia hali hiyo, Samia amewataka wanaCCM, hasa vijana, kutokubali kuchokozeka, badala yake wahakikishe wanafanya kampeni za kistaarabu na kuzingatia muda wa kumaliza mikutano yao ili kutoutia dosari ushindi wao.
Aliyasema hayo juzi jioni katika mikutano yake ya kampeni aliyoifanya kwenye majimbo ya Kishapu na Shinyanga Mjini, ambayo ilihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi, hali inayodhihirisha imani yao kwa CCM.
Samia alisema ana hakika CCM itashinda kwa kishindo cha zaidi ya asilimia 90, hivyo aliwataka wanachama kufanya kampeni za kistaarabu.
Alisema tayari waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje wameshaanza kufuatilia mikutano yao, hivyo aliwataka wawe makini wasije kuona dosari yoyote.
Kuhusu suala la kufanya kampeni kwa kutumia magari, Samia alisema ameamua kutumia njia hiyo ili aweze kukutana na wananchi kwa urahisi.
Samia alisema hawezi kutumia chopa kwa sababu atashindwa kukutana nao na kubaini changamoto zinazowakabili.
Alisema kitendo cha kutumia usafiri wa barabara kunatoa fursa ya kukutana na wananchi katika maeneo ambayo hayajapangiwa mkutano, ambao wamekuwa wakizuia msafara wake na kupata nafasi ya kueleza changamoto zao ili ziweze kutatuliwa.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Shinyanga Mjini, Stephen Masele alisema amefurahishwa na mafuriko yaliyofanywa na wananchi wa jimbo hilo katika uwanja wa Shycom, hali inayoonyesha ushindi mkubwa kwa CCM.
Mbali na mafanikio yaliyopatikana katika jimbo hilo, alimuomba Samia mara serikali ijayo itakapoingia madarakani, kuwajengea soko la kisasa ili kuwawezesha wafanyabiashara kuwa na eneo la uhakika la kufanyia shughuli zao.
Pia, aliomba kodi zinazotozwa kwa wafanyabiashara kufanyiwa uchunguzi kwa sababu nyingi ni kero kwa wananchi kwa kuwa hazilingani na biashara husika, hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa wahusika.
Masele, pia aliiomba serikali kutoa ruzuku kwa mradi wa maji wa Kashuwasa kwa sababu wananchi wa Shinyanga wanalazimika kulipa bili licha ya mradi huo kuhudumia mikoa mingine.
Alisema gharama za kuendesha mradi huo ni kubwa, hivyo aliomba utengewe ruzuku kwa ajili ya kulipa umeme na ununuzi za dawa ili kuwapunguzia wananchi mzigo.
Samia alisema suala la changamoto za miradi ya maji anazipokea na atazifanyia kazi kuhakikisha wananchi wanapunguziwa mzigo wa gharama na atasimamia hilo kwa kuwa ni kipaumbele chake cha kwanza.
Kuhusu soko, alisema litajengwa kwa sababu ilani inaelekeza ujenzi wa masoko katika maeneo mbalimbali nchini ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika maeneo maalumu, hivyo aliwataka wawe na subira.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Kishapu, Suleiman Nchambi, alisema hana shaka na ushindi kwa CCM kutokana na kufanikisha utekelezaji wa ilani, jambo linalofanya wananchi wazidishe imani kwa chama.

No comments:

Post a Comment