Saturday, 10 October 2015

UKAWA SASA KIWEWE

 
MWANDISHI WETU
KUNDI  la vyama vya upinzani linalojitambulisha kwa jina la UKAWA, sasa limeanza kuweweseka baada ya kupoteza matumaini kutokana na ngome za Arusha na Kilimanjaro kuvunjwa na CCM.
UKAWA walikuwa wakitegemea kuwa mikoa hiyo niyo ngome kubwa na walitarajia zingewainua katika kupata kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 25, mwaka huu.
Hata hivyo, matumaini hayo yameyeyuka baada ya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kuvunja ngome hizo alipokuwa katika ziara za kampeni mapema na katikati ya wiki hii.
Dk. Magufuli alifanya mikutano mikubwa ya hadhara katika miji ya Arusha na Moshi ambayo wataalamu wa masuala ya siasa wanaielezea kuwa ilivunja rekodi za mikutano yote ikiwemo ile ya wapinzani kupitia mgombea wa CHADEMA, Edward Lowassa.
Kutokana na hali hiyo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema hatua hiyo imewafanya viongozi wa upinzani kuingiwa na wasiwasi na hata kuanza visingizio vya kuibiwa kura.
Amesema tayari wamebaini kila dalili ya ushindi wa CCM katika uchaguzi huo na kwmba hiyo ndiyo sababu inayowafanya waweweseke na kutafuta namna ya kuwaeleza wafuasi wao.
Akizungumza kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika jana katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke Dar es Salaam, Dk. Nchimbvi alisema kila kona hivi sasa wapinzani wamekuwa wakitoa madai kwamba kunaweza kutokea mchezo mchafu wa kuibiwa kura huku wakifahamu fika kwamba fursa hiyo haipo.
“Kura hizo zitaibwa wakati gani? Kura zinahesabiwa vituoni na kubandikwa papo hapo. Katika kila kituo cha kupigia kura kuna mawakala wa wagombea wa vyama vyote sasa unaweza kujiuliza kura zitaibwa wakati gani?” alihoji Dk. Nchimbi.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi CCM ina kila sababu ya kushinda uchaguzi wa mwaka huu kutokana na mambo makubwa iliyoyafanya jambo ambalo kila Mtanzania aliye na akili timamu analiona.
Alisema pamoja na mambo mengine, CCM imejihakikishia ushindi kutokana Dk. John Magufuli kuwa mtu anayekubalika na Watanzania wote kutokana na rekodi yake katika utendaji na uadilifu.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema ushindi wa CCM katika uchaguzi wa mwaka huu utaletwa na wapigakura vijana waliohamasika na mwenendo wa Chama katika mambo mbalimbali ikiwemo umakini wake katika kuteua mgombea wake wa urais.
Shaka alisema dhana iliyokuwa ikinadiwa awali kwamba CCM ni Chama kinachofuatwa na wazee pekee, hivi sasa haipo kwa CCM imethibitisha kwamba ni chama cha kila rika kutokana na mfumo wake wa uteuzi wa wagombea ambapo kwa kiasi kikubwa vijana wamepewa nafasi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Sadifa Juma Khamis, alisema aliwataka Watanzania kuwa makini katika kuchagua viongozi imara kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuwa ndio watakaotoa hati ya maendeleo ya nchi.
Akimzungumzia mgombea urais wa CHADEMA, Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, alisema kukatwa kwake katika nafasi ya urais kulitokana na msimamo wa Chama kutaka mgombea mwenye uwezo na anayeuzika.
Sadifa alisema CCM ingekuwa na wakati mgumu katika uchaguzi wa mwaka huu kama ingemsimamisha Lowassa ambaye anaonekana amechafuka kila kona ya nchi.
“Lowassa amechafuka mno, hakuna sabuni ya kumsafishia. Urais ni nafasi kubwa inayohitaji mtu makini kuweza kuimudu,” alisema.
Akizungumza kwenye mkutano baada ya kutambulishwa, Mgombea udiwani wa kata Mbagala Kuu kwa tiketi ya CCM, Yusuph Manji alisema anamshangaa Lowassa kukimbilia upinzani baada ya kukatwa na CCM.
“Kila mmoja anakumbuka kwamba mwaka 2005 alitoa maagizo nikatwe licha ya kushinda kwenye kura za maoni nilipowania ubunge jimbp la Temeke.
“Mimi nilivumilia kwa kuwa nilitambua kuwa hiyo ndiyo demokrasia lakini nashangaa kwa nn yeye leo hii amekimbia,” alisema.
Mkutano huo maalumu uliandaliwa kwa ushirikiano wa UVCCM na Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa lengo la kuwahamasisha wananchi wa Temeke na majimbo yake kuchagua viongozi wa CCM kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kuiletea nchi maendeleo.
SENDEKA: RAIS NI MAGUFULI
Naye mjumbe wa kamati ya kampeni ya ushindi kwa CCM, Christopher Ole Sendeka, amesema mgombea urais kupitia CHADEMA, Edward Lowassa, anajua kwamba rais wa awamu ya tano ni Dk. John Magufuli,  baada ya kuvunjwa kwa ngome zao kanda ya Kaskazini.
Amesema mbali na Lowassa hata Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR, James Mbatia, wote wanahafamu kwamba mgombea wao hana uwezo kushinda katika kinyang'anyiro hicho kutokana na imani kubwa waliyo nayo wananchi dhidi ya CCM baada ya kutekeleza Ilani kwa vitendo.
Amesema imani ya wananchi dhidi ya CCM imeongezeka baada ya wachovu kuondoka ndani ya Chama wakiongozwa na Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye na wengine, hivyo imekuwa sawa na kuvuja kwa pakacha na ni nafuu kwa mchukuzi.
Sendeka aliyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi ya Sengerema.
Aliwataka wananchi hao kumchagua Dk. Magufuli kwa kuwa ndiye mgombea pekee wa nafasi hiyo mwenye nia na dhamira ya dhati ya kuwatumikia.
" Watanzania wameshaamua na tayari wamefanya uamuzi na wanachosubiri ni tarehe 25 mwezi huu ili waweze kumthibitisha Dk Magufuli kuwa rais hivyo na ninyi msitetereke. Isitoke hata kura moja, zote zibaki njia kuu ambayo ni CCM kwani michepuko si dili," alisema.
Alisema Lowassa hafai kuwa rais na hata CCM ingempitisha yeye asingekuwa tayari kushirikiana naye. Aliwataka wananchi hao kutodanganyika na kumchagua rais ambaye anaendekeza masuala ya ubaguzi yakiwemo ya kidini.
SAMIA AWAPA NENO
Kwa upande wake Samia alisema serikali ijayo kupitia ilani ya uchaguzi imejipanga kuhakikisha unawezesha wananchi kiuchumi ambapo aliwaahidi kivuko kikubwa katika eneo la Busisi kutokana na msongamano uliopo.
Alisema kivuko hicho ambacho kitakuwa kikubwa zaidi ya mv Sengerema kitaondoa foleni, hivyo wafanyabiashara wataweza kuwahisha bidhaa zao Mwanza na kurahisisha upatikanaji wa masoko.
Kuhusu kuboresha elimu elimu, alisema serikali ijayo imepanga kujenga mabweni katika shule zote kwa kushirikiana na halmashauri husika na wazazi ili kuwawezesha wanafunzi hasa wa kike kusoma katika mazingira bora na kupunguza usumbufu na vishawishi wavipatavyo kwa kutembea umbali mrefu kwenda shule.
Awali akitokea Mwanza kwenda Sengerema aliposhuka katika kivuko cha mv Sengerema katika eneo la Busisi, msafara wake ulisimamishwa na umati wa wananchi waliotaka kumsikiliza na kumwomba awasaidie kuwatatulia kero ya maji inayowakabili.

No comments:

Post a Comment