Saturday 10 October 2015

MSUKUMA AMLIPUA SUMAYE, ASEMA NDIYE CHANZO CHA MIKATABA MIBOVU YA MADINI


NA KHADIJA MUSSA, MWANZA
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma, amemshukia Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye na kumtaka aache uongo kwa kuwaambia wananchi kuwa atahakikisha atawarudishia machimbo ya madini  ndani ya siku 100.
Amesema kiongozi huyo ameonyesha uongo na hadaa za hali ya juu  wakati  ndiye chanzo cha mikataba mibovu ya madini ambayo inalitesa taifa.
Msukuma amesema Sumaye alipokuwa Waziri Mkuu, alitia saini mikataba ya madini ambayo  ukomo wake haueleweki, hivyo kuhoji atawezaje kurudisha machimbo hayo kwa wananchi.
Msukuma aliyasema hayo juzi jioni alipozungumza na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni wa Mgombea Mwenza wa Urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyabulugoya, jimbo la Nyamagana.
Alisema Sumaye aache kuwadanganya wananchi kwamba wakiichagua CHADEMA atawezesha kurudisha machimbo mikononi mwao jambo ambalo haliwezekani na yeye ndiye aliyelisababishia taifa hasara kwa kutia saini mikataba mibovu, hivyo aliwataka watu wampuuze.
Kuhusu kitendo cha aliyekuwa kada wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru kuhamia Chadema,  kwa madai kwamba anataka mabadiliko, alisema kama kweli anayataka basi ayafanye kwa kuanza kurudisha fedha za umma alizokuwa anakusunya katika Kutuo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoa na nchi jirani cha Ubungo, jijini Dar es Salaam badala ya kuwalaghai wananchi.
SENDEKA: AMEPOTEZA MELEKEO
Mjumbe wa kamati ya kampeni ya ushindi ya CCM, Christopher Ole Sendeka, alimshukia Kingunge na kusema amepoteza mwelekeo kwa sababu awali alijifanya mtu wa kufuata misingi na mlengo wa ujamaa na kujitegemea na alikuwa anafundisha kuifuata lakini kwa sasa imebadilika na kujiunga na chama cha mabwanyeye.
Pia alimtaka aeleze umma sababu za kuwa na mapenzi na mgombea wa urais kupitia CHADEMA, Edward Lowassa kwa sababu  alikuwa miongoni mwa viongozi walioshiriki katika kikao cha kilichomwondoa Lowassa katika kinyang'anyuro cha urais mwaka 1995.
Sendeka alisema Kingunge analalamika kuwa Lowassa hakutendewa haki kwa kukatwa jina lake bila ya kuhojiwa na yeye si kwanza kwa kuwa tukio kama hilo liliwahi kumtokea aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, John Malecela ambaye alienguliwa katika kinyang'anyiro kama hicho na hakusikika alilazimika iweje leo.
Alisema Lowassa si mtu wa kumpa nafasi ya uongozi ni msaliti na kamwe hatowaketea maendeleo kwa sababu ni mbinafsi na mroho wa madaraka.
Kuhusu Sumaye alisema amekubali kujiunga na CHADEMA ili aweze kutumika kwa ajili ya akiba iwapo Lowassa atashindwa kuendelea hivyo amewekwa kama tairi la akiba.

No comments:

Post a Comment