Saturday, 10 October 2015
BODABODA WAIKACHA CHADEMA, WAJIUNGA CCM
Na Mwandishi Wetu
Zaidi ya waendesha bodaboda 500 katika Jimbo la Ubungo, Dar es Salaam, wamegeuka na kuahidi kuwa wanachama watiifu wa CCM.
Waendesha bodaboda hao walichukua uamuzi huo, baada ya kupewa elimu kuhusu sababu za kuzuiwa kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Hatua hiyo imekuja kutokana na jitihada kubwa iliyofanywa na mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Ubungo, Dk. Didas Massaburi, ambaye pia ameahidi kuwasilisha hoja binafsi bungeni endapo atachaguliwa ili sheria hiyo ifutwe mara moja.
Dk. Massaburi aliweka hadharani kwamba sheria inayowazuia waendesha bodaboda kuingia katikati ya Jiji, ilitayarishwa mwaka 2008, wakati mgombea urais kupitia Chadema na Ukawa, Edward Lowassa akiwa Waziri Mkuu na Mbunge wa Ubungo aliyemaliza muda wake, John Mnyika, alishiriki kuipitisha mwaka 2011 ndani ya Bunge.
Baada ya kuahidiwa kufutwa kwa sheria hiyo, kuanzishiwa Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) cha waendesha bodaboda, na kuondolewa kwa kero zao mbalimbali na ushuru, zaidi ya vijana 500 walilipuka kwa furaha na wote waliomba kukabidhiwa kadi, bendera na fulana za CCM na kujitangaza kuwa wanachama waaminifu.
Mkutano huo baina ya waendesha bodaboda hao na Dk. Massaburi uliomalizika kwa kutolewa kwa maazimio mbalimbali ya kuwasaidia waendesha bodaboda, ulifanyika katika Ukumbia wa Sisimizi, eneo la Manzese, jana, ambapo pia walimwomba Dk Massaburi kuwa mlezi wao.
Benson Mwakalenga, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema waendesha bodaboda wamekuwa wakifanya kazi zao katika mazingira magumu ikiwemo kuzuiwa kuingia katikati ya Jiji na pia kukumbana na usumbufu mkubwa katika taa za Ubungo, huku wanaofanya vitendo hivyo wakimsingizia Dk Massaburi kutoa amri hiyo akiwa Meya wa Jiji.
Dereva mwingine, Richard Kessy wa Mabibo pia alimwomba Dk. Massaburi kutoa ufafanuzi juu ya zuio hilo la waendesha bodaboda na baada ya kuridhishwa na ufafanuzi wa Dk. Massaburi, aliwaomba wenzake kumchagua kuwa mlezi wa umoja wao akisema hakuna mahali aliposhiriki kuandaa zuio hilo la Bunge.
Alisema si sahihi kumhusisha Meya wa Jiji la Dar es Salaam na zuio hilo kwa vile si kweli kwamba Sheria ya Kuzuia Bodaboda Katikati ya Jiji la Dar es Salaam iliundwa na Halmashauri ya Jiji kwa vile halmashauri zinahusika na sheria ndogondogo na si zile zinazopitishwa na Bunge na kuhusisha nchi nzima.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa CCM alisema akishinda ubunge, pia ataondoa kero zote za waendesha bodaboda na aliahidi kusimamia uanzishwaji wa SACCOS ambayo itawawezesha kukopa bodaboda na kuwawezesha kuendesha zao binafsi, ambapo kwa kuanzia alisema atatoa bodaboda 20 mara moja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment