DK. Magufuli akiwahutubia wananchi baada ya kuusimamisha msafara wake eneo la Igoma mjini Mwanza |
DK. Magufuli akihutubia wananchi waliomsimamisha eneo la Kisesa mjini Mwanza |
Dk. Magufuli akipanda juu ya gari ili aweze kuwahutubia wananchi waliomsimamisha barabarani eneo la Kwimba |
Dk. Magufuli akinadi sera zake kwa wananchi wa Kwimba |
Wananchi wakimsikiliza Dk. Magufuli baada ya kusimamisha msafara wake eneo la Mabatini mjini Mwanza |
Dk. Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika jimbo la Magu |
Na Rashid Zahor, Mwanza
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema ili serikali yake ya awamu ya tano iweze kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM, atalazimika kuteua waziri mkuu mchapakazi.
Dk. Magufuli amesema waziri mkuu huyo ndiye atakayekuwa kiongozi na msimamizi mkuu wa shughuli za serikali, hivyo anapaswa kuwa mchapakazi hodari na makini ili awe mfano wa kuigwa na mawaziri wengine.
Aidha, Dk. Magufuli amesema hatakuwa na huruma na mtendaji yeyote wa serikali, ambaye atashindwa kutekeleza maagizo yake kwa wakati. Alisema iwapo atatokea mtendaji wa aina hiyo, atamtimua kazi mara moja.
Dk. Magufuli alisema hayo jana, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni, uliofanyika eneo la Sokoni, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.
Kabla ya kuhutumia mkutano huo wa kampeni, Dk. Magufuli alilazimika kuhutubia mikutano isiyo rasmi 19 kutokana na msafara wake kusimamishwa na wananchi wakati ulipokuwa ukipita katika maeneo mbalimbali.
Dk. Magufuli ametoa ahadi ya kuteua waziri mkuu mchapakazi siku chache baada ya kuahidi kuwa baraza la mawaziri atakaloliunda baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linakuwa na mawaziri wanaofanana naye kiutendaji
Alitoa ahadi hiyo mwanzoni mwa wiki iliyopita, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni, uliofanyika katika Jimbo la Kisarawe, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Katika mkutano huo, Dk. Magufuli alisema hatakuwa tayari kuwateua mawaziri ambao kazi yao itakuwa ni kukaa tu ofisini na kuandika madokezo, badala yake atateua mawaziri wachapazi na atakuwa akifuatilia utendaji wao wa kazi kwa karibu.
Alisema kabla hajamteua mtu kuwa waziri, atamuuliza kwanza iwapo ataiweza kazi hiyo na kwamba iwapo atasema anaweza, atamtaka atiesaini fomu maalumu ya makata. Alisisitiza kuwa, iwapo hawezi, anapaswa kusema mapema kabla ya uteuzi.
"Nataka kama ni waziri wa maji, atembelee miradi ya maji, sio kukaa ofisini. Na kama ni waziri wa elimu, atembelee wanafunzi aone matatizo yanayowakabili. Serikali yangu itakuwa ya kazi tu," alisema Dk. Magufuli katika mkutano huo wa Kisarawe.
Katika mkutano wake wa jana uliofanyika Magu, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi wa wilaya hiyo, serikali yake itazishughulikia changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji.
Alisema tayari hatua za awali za kuanzisha mradi wa maji katika wilaya hizo zimeshaanza, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa mshauri elekezi, ambaye ameanza kufanya upembuzi yakinifu.
"Hili suala la maji niachieni mimi, nitajitahidi kulibeba. Katika kazi zangu huwa sikubali kushindwa. Nataka kuibadili Magu,"alisema mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi hao.
Aidha, aliahidi kuwa serikali yake itajenga barabara ya Magu/Kwimba kwa kiwango cha lami, ikiwa ni pamoja na za maeneo mengine ya eneo hilo, ili ziweze kutumika kwa ajili ya malori, mabasi na magari madogo.
Dk. Magufuli pia aliahidi kuinua kilimo cha pamba na kupandisha bei ya zao hilo ili wananchi wa wilaya hiyo na zinginezo zinazolima pamba nchini waweze kunufaika kimaisha.
Alisema Tanzania imejaliwa kuwa na raslimali nyingi, zikiwemo bahari, maziwa, mifugo na madini, hivyo wananchi wake hawapaswi kuendelea kuishi wakiwa masikini.
Hata hivyo, Dk. Magufuli aliwaeleza wananchi hao kuwa, ili yote hayo yaweze kufanikiwa, wanapaswa kumpigia kura kwa wingi yeye, wabunge na madiwani wote wa CCM ili waweze kufanyakazi kwa ushirikiano.
"Kama watatokea watu kuwahonga siku ya kupiga kura, kuleni kwa mafisadi lakini kulala kwa Magufuli,"alisema.
Mgombea huyo aliwaambia wananchi hao kuwa mikoa yote aliyotembelea hadi sasa, imemuhakikishia ushindi wa kishindo, hivyo kumfanya awe na uhakika mkubwa wa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati akimtambulisha mgombea ubunge wa Jimbo la Magu, Deusdedit Kiswaga kwa wananchi, Dk. Magufuli alinogewa na wimbo wa kumkaribisha mbunge huyo, ulioimbwa kwa lugha na mahadhi ya kisukuma na kuomba urudiwe zaidi ya mara mbili.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Ngudu, wilayani Kwimba, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi kuwa, atakapochaguliwa kuwa rais, atamwagiza waziri wake wa kilimo kushughulikia suala la bei ya pamba.
Alisema lengo la serikali yake ni kuhakikisha kuwa, wakulima hawauzi pamba nje ya nchi, badala yake itajenga viwanda kwa ajili ya kutengeneza nguo hapa hapa nchini.
Mgombea huyo pia alisema serikali yake itatilia mkazo uanzishaji wa viwanda vya ngozi ili viatu navyo viweze kutengenezwa nchini.
Msafara wa Dk. Magufuri ulianza safari ya kwenda Magu saa 2.30 asubuhi, lakini ulifika huko saa saba mchana kutokana na kusimamishwa mara 19 na wananchi waliokuwa na kiu ya kumuona na kumsikiliza.
Alianza kusimamishwa katika eneo na Mabatini, ambapo wananchi walilizingira gari lake na kulilazimisha kusimama ili waweze kumuona na kusikiliza sera zake.
Masafara wake ulisimamishwa tena eneo la Nyakato, ambako wananchi walijipanga barabarani huku wakipunga hewani bendera na mabango ya Dk. Magufuli na kuimba wimbo wa 'rais, rais, rais.'
Moja ya vituko vilivyomvutia Dk. Magufuli akiwa eneo hilo ni mmoja wa kinamama kutoka nyumbani kwake akiwa amejifunga taulo kiunoni na kanga begani na kulisogelea gari lake. Huku akiwa anacheka, mgombea huyo alimzawadia mama huyo kofia yenye nembo ya CCM.
Msafara wa Dk. Magufuli ulisimamishwa tena eneo la National, ambako kundi la vijana lilifunga barabara na kuanza kupiga push-up. Ilibidi Dk. Magufuli asimamishe msafara wake na kuwahutubia.
Hali iliendelea kuwa hivyo wakati msafara huo ulipofika katika eneo la Igoma, ambako umati wa vijana ulilizingira gari lake na kuimba 'Baba mwenye nyumba,' 'rais, rais, rais.'
Wananchi hao waliendelea kuusimamisha msafara wa Dk. Magufuli katika maeneo ya Kisesa, Nyanguge, Duguye, Kahangala na Ilungu.
Katika mikutano hiyo, ambayo haikuwa rasmi, Dk. Magufuli aliwataka wananchi hao kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi mkuu, uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, na kuwapigia kura wagombea wote wa CCM.
Aidha, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hasa katika masuala yanayohusu elimu bure ya msingi na sekondari, mikopo ya sh. milioni 50 kwa wanawake na vijana na dhamira yake ya kufuta ushuru ili kuwapa wananchi unafuu wa maisha.
Akiwa njiani kwenda Ngudu, wilayani Kwimba, Dk. Magufuli alilazimika kusimamisha tena msafara wake katika maeneo ya Kabila, Maligisu, Kadashi, Mantare na Sumvua, ambako mamia ya wananchi walifurika barabarani, wakiwa na shauku ya kumuona na kumsikiliza.
Msafara wa Dk. Magufuli uliendelea tena kusimamishwa katika maeneo ya Nyamilama na Gungumalwa, ambako aliwahutubia wananchi kabla ya kwenda Jimbo la Misungwi, wilaya ya Misungwi, ambako alihutubia mkutano wake wa mwisho wa kampeni kwa siku ya jana.
Katika mkutano huo, Dk. Magufuli aliwahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kuhusu kuwapatia huduma ya uhakika ya maji safi na salama, ujenzi wa barabara za kiwango cha lami na kuimarisha vivuko.
No comments:
Post a Comment