Monday, 26 October 2015

UCHAGUZI WAFANYIKA KWA AMANI



NA MWANDISHI WETU

MAENEO mengi ya Jiji la Dar es Salaam, jana yalitawaliwa na hali ya utulivu na usalama, huku wananchi wengi wakijitokeza kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Licha ya kuwa na hali hiyo, katika jiji hilo, maduka mengi yalikuwa yamefungwa, huku kukiwa na idadi ndogo ya magari barabarani, yakiwemo ya abiria, tofauti na siku nyingine.

Mbali na hayo, katika jiji hilo ambalo siku zote wafanyabiashara ndogo ndogo, maarufu kama wamachinga ambao wamekuwa wakionekana katika mitaa mbalimbali, hususan Kariakoo, jana  hawakuonekana mitaani.

JIMBO LA SEGEREA

Upigaji  kura kwenye baadhi ya maeneo mkoani Dar es Salaam ulikwenda vizuri, huku maeneo mengine yakikumbwa na changamoto ya idadi kubwa ya wapigakura wasiokuwa na uelewa kuhusu uwepo wa majina yao katika daftari la kudumu la wapigakura.

Uhuru ilishuhudia baadhi ya maeneo katika jimbo la Segerea, ambalo lina jumla ya kata tisa.

Katika jimbo hilo, gazeti hili lilishuhudia wasimamizi wa uchaguzi wakikaa bila shughuli ya kufanya kwa dakika zaidi ya 10, kusubiri wapigakura kuhakiki majina yao yaliyokuwa yamebandikwa kwenye vituo hivyo, siku nane zilizopita.

Kitendo hicho kilisababisha uchelewaji wa upigaji kura, hivyo kuhatarisha idadi kubwa ya wananchi kukosa haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kutokana na kikomo cha muda ambao ni saa 10 jioni.

Wakizungumza na gazeti hili, wasimamizi wa uchaguzi katika kata ya Tabata, walisema wananchi wamekuwa wazembe kwa kupuuza maagizo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), yaliyotolewa kwa nyakati tofauti wiki mbili zilizopita, yaliyowahimiza kuhakiki majina yao vituoni.

“Ninashangaa wananchi walikuwa wakihimizwa mara kwa mara kwa namna mbalimbali kuja kwenye vituo hivi au kupiga simu NEC ili kujua kama majina yao yapo au la.

“Lakini hawakufanya hivyo, leo (jana) ndio wanakuja kuhangaika na daftari…badala tuanze mara moja inabidi tuwasubiri,” alisema Sanga Emmanuel.

Kwa upande wa wananchi, walikiri uzembe kwenye suala hilo, lakini walisema hawana wa kumlaumu kutokana na jinsi NEC walivyojipanga kusimamia kuanzia maandalizi mpaka siku yenyewe.

Gazeti la Uhuru lilishuhudia idadi kubwa ya wananchi wakijitokeza kwenye vituo vya kupiga kura kwa amani, huku wakifuata sheria zote za uchaguzi, zikiwemo za kutovaa sare za chama chochote cha siasa.

Aidha, wasimamizi waliopewa mamlaka ya ulinzi na usalama kwenye vituo hivyo kwa nyakati tofauti walisema wananchi wamekuwa watulivu tangu kuanza kwa upigaji kura saa moja asubuhi.

Walisema waliotaka kusababisha vurugu walielekezwa na waongozaji kutoka NEC, hivyo hali kuendelea kuwa shwari.

JIMBO LA ILALA

Katika kata ya Upanga Mashariki, changamoto iliyojitokeza ni ya baadhi ya wananchi kushindwa kupiga kura baada ya majina yao kutoonekana katika daftari la wapiga kura.

Akizungumza katika kituo hicho, msimamizi wa uchaguzi ambaye alikataa jina lake kuandikwa gazetini,  alisema baadhi ya wananchi ambao hawakuhakiki majina yao mapema  na kujikuta wakipata usumbufu wa kutoona majina yao.

Alisema kwa mujibu wa utaratibu uliopo na maelekezo waliyopewa, mwananchi mbaye jina lake halipo katika daftari la wapiga kura, haruhusiwi kupiga kura.

Mbali na hilo, alisema katika mchakato huo wamekutana na changamoto ya mihuri inayotumika kugongea karatasi za wagombea ilileta shida, hivyo waliwasiliana na viongozi husika ili waweze kutafutia ufumbuzi jambo hilo.

Kuhusu vifaa vya kupigia kura, zsimamizi huyo  alisema vilifika kwa wakati na kumekuwa na utulivu mkubwa licha ya kasoro ndogondogo zilizojitokeza.

JIMBO LA KIGAMBONI

Katika vituo vingi kwenye jimbo la Kigamboni hali ya upigaji kura ilikuwa shwari na mwamko wa wananchi kujitokeza umekuwa mkubwa.

Msimamizi Msaidizi, Johnson  Makalanga, alisema hali ya upigaji kura tangu kufunguliwa kwa vituo ilikuwa shwari na kwamba kasoro ndogo zilifanyiwa kazi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni kuharibika kwa vifaa, ikiwemo mihuri, hivyo kusababisha baadhi ya maeneo upigaji kura kuchelewa.

Pia baadhi ya wapigakura walilalamika kukosekana kwa majina yao, jambo lililosababisha sumbufu mkubwa.

JIMBO LA KIBAMBA

Hali katika kata ya Salanga  ilikuwa tete, baada ya mgombea ubunge wa jimbo la Kibamba kupitia CHADEMA, John Mnyika, kudai kuchochea wananchi kuweka kambi kwenye kituo cha kupigia kura cha Kimara Stop Over hadi karatasi za kupigia kura zitakapofikishwa.

Wananchi ambao walichelewa kupiga kura kutokana na uchache wa karatasi za kupigia kura, ambapo kata hiyo ilikuwa inahitaji vitabu 580 kwa kila nafasi ya wagombea.

Baada ya kubainika kasoro hiyo, msimamizi wa kituo hcho aliamua kwenda NEC kwa ajili ya kufuata karatasi hizo.

Zaidi ya magari matatu ya polisi wa kutuliza ghasia yaliwasili kwenye kituo hicho kulinda usalama.

JIMBO LA TEMEKE

Wananchi wengi wa jimbo hilo walijitokeza kwa wingi katika vituo mbalimbali kwa ajili ya kupiga kura, ambapo wengi walionekana wakiwa wanahakiki majina yao, kabla ya kuingia katika vyumba vya kupigia kura.

Vituo ambavyo viliongoza kwa kuwa na watu wengi waliowahi kupiga kura ni vya Sandali, mikoroshini, Tandika, Chang’ombe, Uwanja wa Taifa.

Mgombea ubunge wa jimbo hilo, Abbas Mtemvu kwa tiketi ya CCM, alipiga kura kwenye kata ya Tandika saa 2.10 asubuhi.

Katika jimbo hilo vifaa vyote vilifika kwa wakati sanjari na mawakala wa vyama kwa ajili kuanza wananchi kupiga kura kusimamia kura za vyama vyao.

Hata hivyo, saa 8.30 mchana vituo vingi vilionekana kuwa vitupu baada ya watu kumaliza kupiga kura na hali ilikuwa shwari.

Hata hivyo, katika kata ya Temeke kijana aliyedaiwa kuwa ni mfuasi wa CHADEMA, alikamatwa baada ya kudaiwa kufanya kampeni katika kituo cha kupigia kura.

Pia Issa Amir (18), alikamatwa na polisi baada kugundulika akipiga kura mara mbili katika kituo cha Sandali.

Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Charles Semizigi, alisema Amir alikamatwa wakati akitumbikiza kura ya rais, mawakala waliona kidole chake kikiwa na wino ambao mpigakura huwa anapaka baada ya kupiga kura.

Alisema kuwa wasaidizi walimsaidia kutafuta jina lake mara ya kwanza na akapiga kura na alipokuja tena wakamgundua alishapiga kura.

Hata hivyo, Amir alikana kupiga kura, huku akidai kuwa alikuwa amechezea wino wa peni licha ya kuonekana katika kidole ambacho kinapakwa baada ya kupiga kura.

 JIMBO LA MBAGALA

Upigaji kura katika jimbo jipya la Mbagala, ulifanyika kwa amani na utulivu, huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi.

Hata hivyo, baadhi ya vituo kulikuwa na changamoto, ikiwemo wananchi kutumia muda mrefu kusubiria kuanza kupiga kura katika  kituo cha Kichemchem Shule.

Katika kituo hicho, wananchi walilazimika kusubiri kwa zaidi ya saa mbili, i kutokana na kuchelewa kufika kwa vifaa vya kupigia kura.

Hata hivyo, vijana wengi waliojitokeza walionekana kukata tamaa na kuanza kuondoka baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kuanza kwa zoezi hilo.

Uhuru ilitembelea katika jimbo hilo kwenye maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mission, Kichemchem, Kibonde Maji, Kongowe, Kongowe Shule, Kizuiani, Mbagala Kuu, Nyalu Academy, Nawina na Maji Matitu Shule.

Aidha katika kituo cha Nyalu, kulitokea malalamiko kwa baadhi ya watu kulalamikia majina yao kutoonekana katika orodha ya majina yaliyoandikwa kwa ajili ya kupiga kura.

Baadhi yao kutokuona kwao kulitokana na kutokuwa makini katika uangaliaji wa majina yao, kwani wengi walijitokeza jana badala ya siku chache kabla ya uchaguzi.

JIMBO LA KAWE

WANANCHI wa kata ya Mkwamani katika jimbo la Kawe, waliangua vilio baada ya kukataliwaa kupiga kura kutokana na majina kutokuwepo katika daftari la wapiga kura.

Hatua hiyo ilitokana na majina ya wapigakura hao kutokuwepo kwenye orodha iliyobandikwa kwenye kituo cha kupigia kura.

Hata hivyo, askari waliokuwa wakilinda usalama kwenye kituo hicho waliwataka kuondoka eneo hilo na kwenda kuwasilisha malalamiko yao kwa msimamizi na ofisa mtendaji.

Vituo vingine katika jimbo hilo vikiwemo Tegeta A, Bunju B, Mikocheni B, Shule ya Msingi Ushindi Mikocheni, hali ilikuwa shwari na vifaa vilifika kituoni kwa wakati.

JIMBO LA UBUNGO

Wananchi wa jimbo la ubungo walijitokeza kwa wingi kupiga kura, huku changamoto kwa baadhi ya wananchi kushindwa kupiga kura baada ya majina yao kutoonekana kwenye orodha ya wapiga kura, ikijitokeza.

Licha ya changamoto hiyo, makarani wa uchaguzi pamoja na mawakala wa vyama vya siasa walipata wakati mgumu kuwatuliza  baadhi ya wananchi walioshindwa kuona majina yao.

Vituo vya wapiga kura vilivyotembelewa na gazeti hili ni Ubungo kata, Shule, Kisiwani, Makuburi. Vituo vingine, Msewe, National Housing na Ubungo Kisiwani, ambako wananchi walipiga kura kwa amani na utulivu

JIMBO LA BUKOBA MJINI

Dk. Aman atiwa mbaroni

POLISI mkoani Kagera wanamshikilia mgombea udiwani wa kata ya Kagondo kwa tiketi ya NCCR-MAGEUZI, Anatory Aman, kwa tuhuma za kuvamia kituo cha kupigia kura na kumpora vitabu vya kupigia kura msimamizi wa uchaguzi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, alisema saa 5:40 asubuhi alivamia kituoni hapo bila kutoa taarifa kwa msimamizi wa uchaguzi wa kituo na kuchukua vitabu hivyo kwa madai ya kutaka kuvifanyia ukaguzi baada ya kupata taarifa kuwa kuna kurasa zimechomolewa.

“Hatuhitaji upelelezi zaidi, kwani kafanya kosa hilo mchana kweupe…vurugu kwenye vituo havitakiwi kwa sababu upigaji kura ulisimama kwa saa mbili,” alisema.

Kwa upande wake Msimamzi wa Uchaguzi wa Jimbo la Bukoba Mjini, Aron Kagurumjuli, alisema mgombea hana mamlaka ya kugusa vitabu na kitendo cha kuvamia kituo ni kosa kisheria.

Hata hivyo, Aman alipoulizwa kuhusiana na hatua ya kuvamia kituo na kupora vitabu, alisema alivishika tu na kamwe hakupora.

No comments:

Post a Comment