Wednesday, 28 October 2015

ZEC: MAALIM SEIF ACHUKULIWE HATUA ZA KISHERIA




NA MWANDISHI WETU,  ZANZIBAR
TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), imesema uamuzi wa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza ameshinda uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita, ni kosa kisheria na umesababisha uvunjifu wa amani.

Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Bwawani Hoteli, jana, alisema alichokifanya Maalim Seif ni hatari kwa amani ya nchi.
Alikiri kuwa ZEC imesikia kauli hizo kwenye vyombo vya habari kuhusiana na Maalim Seif kujitangazia matokeo na kwamba, hawana uwezo wa kumkamata na kumfungulia mashitaka na kuvitaka vyombo vya dola kufanyakazi yake.
"Amevunja kifungu cha Sheria ya Uchaguzi namba 42 ya mwaka 1984. Sheria imetungwa na Baraza la Wawakilishi, tumezungumza asubuhi (jana) tukaona tuliachie vyombo husika vichukue hatua," alisema Jecha.

Alisema Maalim Seif anafanya kosa hilo mara ya pili, hivyo ametaka vyombo husika kuchukua hatua stahiki na kuwaomba wagombea wote kuwa watulivu kwa kusubiri tume itangaze matokeo kwa kuwa ndio yenye mamlaka ya kufanya hivyo.

Jecha aliongeza kuwa leo wataendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, ambao pia huenda Rais wa Zanzibar akatangazwa, baada ya kuhakiki na kujiridhisha kwa kuwa wanaondoka kutoka katika vituo wanaweza kuwa
wamekosea au kuandika takwimu tofauti makusudi.

Maalim Seif juzi aliwaambia waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya CUF yaliyoko Mtendeni, Unguja kwamba ameshinda kwa asilimia 52.87 baada ya kupata kura 200,077 dhidi ya 178,363 za mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein, aliyepata asilimia 47.13, ambapo hatua hiyo imeshtua wengi, kikiwemo CCM ambacho kimelaani na kuitaka ZEC kuchukua hatua.

No comments:

Post a Comment