Saturday 7 November 2015

DK. MAGUFULI ATETA NA KIONGOZI WA CHINA


NA MWANDISHI WETU

TANZANIA imeitaka China kuimarisha uhusiano kwa kuisaidia Tanzania kukua zaidi kiuchumi na kibiashara.

Kwa kufanya hivyo, China itaweza kutimiza azma ya viongozi wa Tanzania ya kuwaletea Watanzania maendeleo zaidi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais Dk. John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam  alipokutana na Zhang Ping, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ambacho ndicho chama tawala nchini humo.

“Tuimarishe uhusiano wetu kwa misingi ya kuufanya uwe uhusiano wa kuisaidia Tanzania kunufaika kiuchumi na kibiashara ili kuweza kutimiza azma yangu ya kuwaletea watanzania maendeleo,” alisema Rais Magufuli.

Taarifa iliyotolewa na Mwandishi Msaidizi wa Habari wa Rais, Premy Kibanga, ilisema Ping alikuja nchini kumuwakilisha Rais wa China katika sherehe za kuapishwa Rais Magufuli, zilizofanyika juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mbali na Ping, Rais Magufuli alikutana na viongozi wengine ambao pia waliwakilisha viongozi wa nchi zao katika sherehe hizo.

Wawakilishi hao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Algeria, Ramtane Lamamra; Spika wa Bunge la Burundi, Pascal Nyabenda na Waziri wa Kilimo wa Misri, Essam Fayed.

Mapema jana, Rais Magufuli alimwapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  George Masaju, kisha kuendelea na kazi zake za kiofisi.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwataka watumishi wote kufanya kazi zao kwa uadilifu, bidii na kujituma zaidi ili kuwatumikia Watanzania na  kutimiza mategemeo yao ya kuletewa maendeleo na kukua kiuchumi.

No comments:

Post a Comment