Saturday 7 November 2015

CCM YAPATA VITI MAALUMU 64 BUNGENI


NA REHEMA MAIGALA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepata idadi kubwa ya viti maalumu kuliko wapinzani, baada ya kupata kura nyingi za ubunge nchini kote.

Katika mgawanyo huo wa viti maalumu, CCM imepata viti 64 huku ikifuatiwa na CHADEMA yenye viti 36 na CUF viti 10.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jaji mstaafu Damian Lubuva, imetoa idadi ya wabunge wa viti maalumu, imetolewa kwa  kwa vyama hivyo baada ya kukidhi vigezo vya Katiba na sheria ya kupata angalau asilimia tano ya kura zote halali za ubunge.

Alisema katika uchaguzi huo, CCM ilipata kura halali za ubunge  8,333,953 huku CHADEMA ikipata 4,627,923 na CUF kura 1,257,051.

Jaji Lubuva alisema uchaguzi wa mwaka huu, ulihusisha majimbo 258 kati ya 264, ambapo CCM ikiwa imeshinda majimbo 182 ikifuatiwa na CUF iliyoshinda majimbo 39,  CHADEMA  35, ACT –Wazalendo na NCCR-Mageuzi moja kila kimoja.

Awali bunge la 10 lilikuwa na wabunge wa majimbo 254 ambapo CCM ilikuwa na viti 186, CUF 23, CHADEMA 24, NCCR-Mageuzi vinne huku UDP na TLP kiti kimoja kimoja.

Alisema NEC imepewa mamlaka ya kutangaza Viti Maalum vya Wabunge wanawake visivyopungua asilimia 30 ya wabunge wote.

Lubuva alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka  huu, viti maalumu ni 113,  lakini kutokana na majimbo manane ambayo hayakufanya uchaguzi,  mgawanyo wa viti maalumu kwa sasa  ni 110.

Alisema viti vitatu vilivyobaki vitagawanywa baada ya kufanyika kwa uchaguzi katika majimbo yatakayorudiwa uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment