Saturday 7 November 2015

RAIS MAGUFULI AFANYA ZIARA YA GHAFLA WIZARA YA FEDHA


NA MWANDISHI WETU

RAIS Dk. John Magufuli, jana alianza kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa kufanya ziara ya kushitukiza katika Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Alitinga katika ofisi hizo, maarufu kama Hazina, muda mfupi baada ya kumwapisha Mwanasharia Mkuu wa Serikali, George Masaju, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Rais alitoka Ikulu kwa mguu na kuingia wizarani hapo kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa watumishi katika wizara hiyo. Ofisi za Wizara ya Fedha ziko mita chache kutoka Ikulu.

Mara baada ya kuwasili, alikutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, na kutia saini kitabu cha wageni.

Baada ya kufanya hivyo, katika hali isiyotegemewa, Rais Dk. Magufuli alitembelea ofisi moja baada ya nyingine na kujionea maajabu. Katika  baadhi ya ofisi alikuta watendaji, wakiwemo maofisa waandamizi, wakiwa nje ya ofisi.

Rais kila alipohoji waliko maofisa hao, hakupata majibu ya moja kwa moja, kumaanisha kwamba walikuwa nje ya ofisi bila taarifa zozote.

Alipofika katika ofisi hizo, alikuwa akiuliza “huyu hapa ni nani na yuko wapi?” huku akiwa hapati majibu ya kuridhisha. Aliendelea vivyo hivyo katika ofisi kadhaa, ambapo wasiokuwepo walikuwa wakiulizwa majina yao na kutajiwa.

Alipomaliza kutembelea ofisi hizo alipata fursa ya kuzungumza na maofisa waandamizi na maofisa wakuu wa wizara.

Jambo kubwa alilozungumza na viongozi na watumishi hao waandamizi ni kuhakikisha wanaziba mianya ya ukwepaji kodi ili kuiwezesha serikali kukusanya mapato mengi.

“Masuala ya kusamehe kodi yawe yale yaliyoko kwenye mikataba tu na wahisani, lakini mengine yasimamishwa kuanzia sasa,” alisema.

Sambamba na hilo, aliiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unaongezwa kwa kasi ili kuiwezesha serikali kupata mapato ambayo pamoja na mambo mengine, yatawezesha serikali kutimiza azma yake ya kutoa elimu bure mpaka kidato cha nne.

Hata hivyo, alisema ukusanyaji wa kodi huo usilenge watu wadogo tu bali hata wale wafanyabiashara wakubwa ambao wanaagiza mizigo nje na kufanya udanganyifu.

“Hakikisheni mnashirikiana na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kuhakikisha mnakusanya kodi. Hii si tu kwa wananyabiashara wadogo wanaouza vitumbua huko chini na kuwaacha wale wanaoleta mizigo wakidai wanaleta gypsum wakati wana TV (televisheni) kwenye makontena yao,” alisisitiza.

Rais Magufuli pia aliwataka mataalamu wa Wizara ya Fedha na wale wa TRA kusimamia ipasavyo uingiaji na utoaji mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ili kudhibiti ukwepaji wa kodi.

Ziara hiyo ya Rais Magufuli katika ofisi hiyo nyeti serikalini, imetafsiriwa na baadhi ya watu kwamba ni mwanzo wa utekelezaji wa yale aliyoyaahidi wakati wa kampeni na hotuba zake alizozitoa hivi karibuni, ikiwemo juzi baada ya kuapa kuwa Rais kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Ofisi Ndogo za CCM Lumumba, Dar es Salaam, alisema hatakuwa na simile ya kutekeleza majukumu yake muda mfupi baada ya kuapishwa.

Hiyo ilijidhihirisha juzi baada ya kuapishwa ambapo muda mfupi alimteua Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu.

No comments:

Post a Comment