Wednesday 18 November 2015

MANJI AFANYA MRADI WA KIHISTORIA ZANZIBAR




NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini na Kampuni ya Quality Group Limited (QGL), mkataba wa ujenzi wa mji wa kisasa katika eneo la Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.
Uamuzi huo wa ujenzi wa mradi mkubwa wa uwekezaji na wa kwanza katika historia ya Zanzibar, unalenga kuinua fursa za ajira, kukuza utalii na uchumi kwa kasi.
Mradi huo ambao utatekelezwa kwa awamu mbili, unatarajiwa kugharimu zaidi ya sh. bilioni 500, ambapo utatoa fursa za ajira kwa Wazanzibar zaidi ya 15,000.
Akizungumza wakati wa kutiliana saini mkataba huo, Mwenyekiti wa Kampuni ya QGL, Yusuf Manji, alisema ameamua kufanya uwekezaji huo mkubwa ili kusaidia juhudi za serikali kukuza uchumi na utalii visiwani humo. Mji huo utajulikana kama Stone Town Village.
Alisema mradi huo utahusisha uboreshaji wa Hoteli ya Bwawani, ambayo itakuwa chini ya usimamizi wa QGL, ujenzi wa nyumba za kisasa 380 na maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali.
Pia, utahusisha sehemu ya maegesho ya magari na michezo ya watoto, masoko kwa ajili ya shughuli za wazawa na wageni na huduma zote za kijamii, ikiwemo hospitali ya kisasa yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 250.
Manji, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, alisema mbali na huduma hizo, pia mradi huo utahusisha ujenzi wa barabara na uzalishaji umeme wa kutosha kwa ajili ya kuhudumia eneo hilo na maeneo ya jirani.
“Zanzibar ni sehemu ya Tanzania na hapa ndipo baba yangu (Mzee Mehbub Manji) alikozaliwa, hivyo nina historia napo nzuri sana. Tunafanya uwekezaji huu mkubwa ili kukuza uchumi na utalii wetu. Hakuna sababu ya watu kwenda Malaysia wakati Zanzibar kuna kila kitu,” alisema Manji.
Aliongeza kuwa mradi huo utaanza utekelezaji wake hivi karibuni kwa kuwatumia wakandarasi wa nje na wazawa, ambao watahusika kwenye hatua mbalimbali na utazingatia sheria zote ikiwemo uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIFA), Salum Nassoro, alisema mradi huo ni wa kihistoria na utasaidia kuongeza kufungua fursa visiwani hapa.
Alisema mbali na kukuza uchumi na kuvutia watalii zaidi, mradi wa Stone Town Village, utaongeza mapato ya serikali na kuitangaza zaidi Zanzibar ulimwenguni kote.
Kuhusu Hoteli ya Bwawani, Nassoro alisema itakarabatiwa na kuwa katika kiwango cha nyota tano na kwamba, taswira yake itaendelea kutunzwa kwa ajili kumbukumbu ya kipekee ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Amri Abeid Karume.
Aliongeza kuwa mradi wa ujenzi wa Stone Town Village utatekelezwa kwa mujibu wa sheria na hautaathiri mandhari ya Mji Mkongwe.

No comments:

Post a Comment