Tuesday 17 November 2015

SHAKA: SHEIN NI KIONGOZI MAKINI



KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, amepongeza uvumilivu , hekima na busara anazotumia  Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein katika  kuiepusha nchi kuingia kwenye vurugu na ghasia
Hata hivyo amevitaka vyama vya upinzani, hususan CUF kutotumia fursa hiyo vibaya kwani CCM inatambua vyema  nyendo zao zinazoashiria kutaka kuiingiza nchi katika machafuko.
Amewataka wana-CCM Zinzibar kujiweka tayari na maandalizi ya  uchaguzi wa marudio, iwapo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), itatangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio baada ya ule wa awali kufutwa uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, kufutwa kisheria.
Akizungumza na makundi ya vijana kutoka majimbo yote ya mkoa wa Kaskazini Unguja , huko  Kinduni, Wilaya ya Kaskazini A, alisema Dk. Shein anastahili pongezi kutokana na  uvumilivu wake na  umekuwa chachu ya kudumisha utulivu na amani ya Wazanzibari wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.
“UVCCM tunampongza kwa dhati Dk. Shein kwa subira, busara na ustahamilivu wake. Ameonyesha ukomavu wa kisiasa na tunatambua bila ya kufanya hivyo, pengine tungekuwa katika hali mbaya ya kiusalama.

“Tunaomba moyo na ustaarabu ulioonyeshwa na Dk. Shein uwe ni somo kwa wanasiasa wote hususan wa upinzani, ambao mara nyingi wamekuwa wakishindwa kufanya hivyo na ushahidi wa wazi ni chokochoko zinazoanzishwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyejitangaza mshindi wa uchaguzi mkuu kabla ya mamlaka zinazohusika hazijafanya kazi yao,”alisema.
Kawa mujibu wa Shaka, wana-CCM wanapaswa kujenga utayari na kuchemsha bongo kuelekea  uchaguzi  wa marudio mara tarehe itakapotangazwa wakati wowote  na ZEC.
Awali, akizungumza katika mkutano na vijana wa CCM wa mkoa wa Mjini, mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Seleman Haji, alisema katika uchaguzi uliofutwa na ZEC, wako baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM waliodiriki kushirikiana na upinzani kwa kutazama maslahi binafsi.
Haji  alisema  utafiti wa haraka  unaonyesha moja ya kuanguka kwa wagombea wa CCM kwenye baadhi ya maeneo, kulichangiwa na tamaa za wana-CCM wasio waaminifu.
Kwa mujibu wa Haji,  jambo hilo linapaswa kupingwa na wana-CCM wote ili lisijirudie katika uchaguzi ujao na Chama kijihakikishie ushindi wa kishindo.
 “CUF waliiba kura kwenye vituo mbalimbali, lakini na sisi wana-CCM wenyewe pia tuwe makini kwa kuwa wapo baadhi yetu wanaoendekeza tamaa na kuwa tayari kukikandamiza Chama ili wapate fedha na maslahi mengine,” alisema.

No comments:

Post a Comment