Wednesday, 16 December 2015
VIGOGO TRA, TPA WAKWAMA KUPATA DHAMANA
NA FURAHA OMARY
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kandaya Dar es Salaam, imetoa mashartiya dhamana kwa vigogo wanane waMamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bandari Kavu ya (ICD) ya Azam, akiwemo Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Mamlaka hiyo, Tiagi Masamaki.
Jaji Winfrida Koroso, alitoa masharti hayo jana alipokuwa akitoa uamuzi kuhusu maombi ya dhamana yaliyowasilishwa mahakamani hapo na Masamaki na wenzake kwa kupitia mawakili wao, Alex Mgongolwa na Majura Magafu.
Masamaki na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, waliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu, kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Katika kesi hiyo, Masamaki na wenzake wanadaiwa kuisababishia serkali hasara ya sh. bilioni 12.7, kutokana na makontena 329 kutolewa katika Bandari ya Dar es Salaam bila ya kulipiwa kodi.
Akitoa uamuzi wa maombi ya dhamana, Jaji Winfrida alisema mahakama imejiridhisha kwanza kuwa ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na baada ya kusikiliza na kuzingatia maelezo ya pande zote mbili, kiapo kilichoambatanishwa na maombi, hoja za mawakili na vipengele vya sheria, mahakama imeamua kuwapa dhamana.
Pia alisema dhamana ni haki yao na kosa linalowakabili lina dhamana. Jaji alimtaka kila mwombaji aweke mahakamani sh. bilioni 2.7 au hati za mali isiyohamishika zenye thamani hiyo.
Alisema waleta maombi hao, walitakiwa watoe nusu ya fedha iliyodaiwa katika hati ya mashitaka, ambayo nusu hiyo imegawanywa kwa waleta maombi wote.
Aidha, Masamaki na wenzake wametakiwa wawe na wadhamini wawili wa kuaminika, watakaotia saini dhamana ya sh. milioni 20 kila mmoja na mmoja kati ya wadhamini hao awe mfanyakazi wa serikali.
Masharti mengine ni Masamaki na wenzake hawatakiwi kusafiri nje ya Dar es Salaam bila ya kibali cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wawasilishe hati zao za kusafiria katika Mahakama ya Kisutu.
Pia wanatakiwa kuripoti kwenye ofisi za mpelelezi wa makosa ya jinai za mkoa kila baada ya wiki mbili. Jaji aliamuru nyaraka zote zitakazotolewa kwa ajili ya dhamana zihakikiwe katika Mahakama ya Kisutu ndani ya saa 24 kuanzia jana.
Mbali na Masamaki, waleta maombi wengine ni Meneja wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya, Msimamizi Mkuu wa ICD-Azam, Eliachi Mrema, Meneja wa Udhibiti wa Forodha na Ufuatiliaji, Bulton Mponezya, Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara TRA, Khamis Omary .
Wengine ni Haroun Mpande wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT–TRA, Meneja Uendeshaji Usalama na Ulinzi wa Azam ICD, Raymond Louis na Meneja Azam ICD, Ashraf Khan.
Baada ya kutolewa kwa masharti hayo, Masamaki na wenzake walirudishwa rumande kwa kuwa wanatakiwa waende kuyatimizia Mahakama ya Kisutu.
Desemba 3, mwaka huu, Masamaki na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama ya kudanganya na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 12.7, kutokana na makontena 329 kukwepa kodi.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, wanadaiwa Tarehe tofauti kati ya Juni Mosi na Novemba 17, mwaka huu, sehemu isiyofahamika katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam, walikula njama pamoja ya kufanya udanganyifu kwa serikali wa sh. bilioni 12.7.
Inadaiwa walidanganya kwa kuwasilisha kwamba makontena 329 yaliyokuwepo katika bandari kavu ya Azam, yametolewa baada ya kulipiwa kodi.
Pia washitakiwa hao wanadaiwa katika kipidi hicho jijini Dar es Salaam, walishindwa kutimiza majukumu yao inavyotakiwa, hivyo kuisababishia serikali hasara ya sh. Bilioni 12.7.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, mbele ya Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na maombi yao ya dhamana wayawasilishe Mahakama Kuu ya Tanzania.
CHANZO CHA HABARI GAZETI LA UHURU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment