Wednesday, 20 January 2016

BOMOABOMOA UTATA MTUPU




BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesisitiza kuendelea na bomoa bomoa katika maeneo ya wazi, mabondeni na kwenye kingo za mito, licha ya vurugu zinazofanywa na baadhi ya wakazi wa maeneo hayo.
Wakati NEMC ikisisitiza hayo, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi, imeamuru hali iendelee kubaki kama ilivyo kwa sasa kwa mkazi wa Misheni Kota, Kata ya Mchikichini, wilayani Ilala, Dar es Salaam, Waziri Kindamba na wenzake 88, ambao wamewasilisha maombi mahakamani hapo.
Akizungumza jana na Uhuru, Mwanasheria Mkuu wa NEMC, Heche Manchare, alisema licha ya usumbufu unaojitokeza, ni lazima watu watoke mabondeni na kwamba serikali  itaendelea na bomoa bomoa si Dar es Salaam tu, bali kwenye maeneo yote ya wazi, mabondeni na kwenye kingo za mito nchini kote, ikiwemo Mlalakuwa, Ruaha, Ihefu na sehemu nyingine.
Heche aliwataka wananchi ambao bado wapo katika maeneo hayo, kuondoka haraka kwa kuwa siku zao zinahesabika na kusema inachokifanya serikali ni utekelezaji wa sheria na si kumwonea mtu yeyote.
Alisema jamii inapaswa kutambua kuwa serikali haiwaondoi wananchi katika maeneo hayo hatarishi na kuyaacha kama yalivyo, bali itayaendeleza kwa matumizi ya umma kama ilivyokwisha kuelekezwa.
Alikiri serikali kufanya makosa miaka iliyopita kwa kutosimamia suala la ujenzi sahihi, lakini alisema kosa hilo halitarudiwa kwa kuwa pia anayo imani na Rais Dk. John Magufuli, katika kusimamia utii wa sheria.
Pia, alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga maeneo kulingana na shughuli maalumu, ikiwemo ya makazi, viwanda, biashara, kupumzikia na shughuli nyingine za umma, ili kuondoa uwezekano wa wananchi kujenga kiholela.
Mbali na hayo, NEMC imeviasa baadhi ya vyombo vya habari, kuacha kuegemea upande mmoja wa malalamiko ya wananchi waliobomolewa, badala yake vijikite kuelimisha jamii juu ya athari za kuishi katika maeneo hayo hatarishi.
Katika hatua nyingine, aliwashukia wanasiasa  kutokana na kauli wanazotoa kuwa wananchi hao wanaonewa na serikali huku baadhi yao wakiwaongoza mahakamani.
Heche alisema bomoa bomoa haijasitishwa isipokuwa serikali inaendelea na tathmini, hivyo ni muda mzuri kwa wakazi hao hususan waliowekewa alama ya X, kuhama kwa hiari kabla ya kuendelea kwa shughuli hiyo.
Wakati huo huo, Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, imeamuru hali iendelee kubaki kama ilivyo kwa sasa kwa mkazi wa Misheni Kota, Kata ya Mchikichini, wilayani Ilala, Dar es Salaam, Waziri Kindamba na wenzake 88, ambao wamewasilisha maombi ya kupatiwa kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi.
Jaji John Mgetta wa mahakama hiyo, ameamuru hali hiyo ibaki hivyo wakati maombi hayo namba 13 ya mwaka huu, yakisubiri kusikilizwa na kutolewa uamuzi Ijumaa wiki hii.
Kindamba amewasilisha maombi hayo namba 13 ya mwaka huu, kwa niaba ya wenzake 88, akiomba apatiwe kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi ili waweze kufungua shauri la kupinga bomoa bomoa katika eneo hilo.
Mkazi huyo amewasilisha maombi hayo dhidi ya
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Kamishna wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mtendaji wa NEMC, ambapo pia anaiomba mahakama kutoa  amri ya zuio la muda dhidi ya wajibu maombi, kuacha kubomoa nyumba zao kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi yao ya kibali.
Maombi hayo yalipangwa kwa Jaji Mgetta, ambaye amepanga Alhamisi wiki hii, atasikiliza maombi ya kibali, zuio la muda na pingamizi la serikali na kutoa uamuzi siku inayofuata.
Jaji Mgetta aliamuru kwamba wakati maombi hayo yakisubiri kusikilizwa, hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi Ijumaa wiki hii atakapotoa uamuzi.
Kwa kupitia hati yao ya maombi, ambayo imeungwa mkono na hati ya kiapo cha wakili wao, Mohamed Majaliwa, mkazi huyo anadai anaomba amri ya zuio la muda na wenzake kwa kuwa ni wamiliki halali wa nyumba zilizoko katika eneo hilo.
Anadai wajibu maombi wanaendesha operesheni ya kuziwekea alama ya X nyumba hizo kama ishara ya kwamba zinatakiwa kubomolewa na kutokana na hali hiyo, ameshafungua maombi ya kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi kwa niaba ya wenzake 88, kupinga bomoabomoa hiyo.

No comments:

Post a Comment