RAIS Dk. John
Magufuli, amesema serikali ya Tanzania itafungua ubalozi wake nchini Israel
muda wowote ili kuendeleza ushirikiano na mahusiano baina ya nchi hizo.
Alisema hayo
alipokutana na Balozi wa Israel hapa nchini, Yahel Vilan, Ikulu jijini Dar es
Salaam, ambako amemhakikishia kuendeleza ushirikiano na kuimarisha mahusiano
yenye manufaa kwa nchi hizo mbili.
Alisema
anatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Israel na umuhimu wake
kwa ustawi wa nchi hizo na kwamba, anataka yaimarishwe zaidi katika kipindi
chote cha uongozi wake.
Kwa upande
wake, Balozi Yahel, alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri
inayoendelea kufanywa na uongozi wake katika kipindi kifupi cha miezi miwili
tangu aingie madarakani.
Alisema kuwa
Israel ina kila sababu ya kuendelea kushirikiana na Tanzania na ipo tayari
kuimarisha zaidi mahusiano ya kidiplomasia kwa manufaa ya pande zote katika
nyanja zote za maendeleo.
Balozi huyo
alitaja baadhi ya maeneo ambayo serikali yake inakusudia kushirikiana na
Tanzania kiuchumi kuwa ni pamoja na kilimo, maji, ufugaji wa nyuki, sayansi na teknolojia.
Pamoja na
hilo, alibainisha kuwa Israel imewaalika Jumuia ya Wafanyabiashara wa Tanzania,
kushiriki katika kongamano la biashara kati ya Tanzania na Israel.
Alisema
kongamano hilo linatarajiwa kufanyika mjini Tel Aviv, nchini Israel, Septemba,
mwaka huu.
Pia, aliahidi
kufikisha ujumbe wa Rais Magufuli kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
pamoja na kuahidi kuanzisha haraka ofisi ya kutoa huduma ya vibali vya
kusafiria hapa nchini kwenda Israel (visa).
No comments:
Post a Comment