SERIKALI
imesema haitawafumbia macho maofisa wa ardhi wanaotajwa kuhusika kwenye kero na
migogoro mbalimbali za ardhi.
Onyo
hilo limetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ambaye amesema mwisho wa
malalamiko na kero za mara kwa mara kwa wananchi dhidi ya maofisa ardhi
zimefika mwisho.
Alikuwa akizungumza mjini hapa juzi, na kuwataka maofisa
wa ardhi nchi nzima, kufanyakazi kwa uadilifu na kutambua kuwa jamii
inawatazama.
“Ofisa ardhi atakayetajwa tena kuhusika na ugawaji
wa kiwanja kimoja kwa watu wawili hatutamuacha,’’ alisisitiza Lukuvi.
Aliwaagiza wakuu wa mikoa kuainisha mashamba ya
mikonge na mengine, ambayo kwa sasa hayatumiki ili yafutiwe hati zao na kupewa
wananchi ili kupunguza migogoro ya ardhi.
Alitoa agizo hilo baada ya kupokea kero za wananchi
wa wilaya ya Kilosa kwamba, yapo mashamba ya mikonge, ambayo kwa sasa hayalimwi
zao hilo, badala yake yanakodishwa kwa wananchi kwa bei kubwa.
‘’Wakuu wa mikoa fuatilieni mashamba kama hayo,
ambayo kwa sasa yameacha lengo
lilioombewa na kutumika katika shughuli nyingine, ardhi ni ya serikali, ‘’
alisema.
Waziri Lukuvi aliwataka wananchi kuacha kuvamia
mashamba na viwanja vyenye hati, badala yake wakiona yametekelezwa,
wafuate taratibu za kuomba kufutiwa hatimiliki.
‘’Ukivamia shamba la mtu, sheria itachukua mkondo
wake, sheria ni msumeno, inauma huku na huku, fuateni taratibu,‘’ alisema.
Hata hivyo, Lukuvi alisema ipo haja kwa wizara yake
na wizara ya maliasili na utalii, kufanya ziara ya pamoja ili kuangalia maeneo,
ambayo sheria zinagongana ili kufanya suluhisho la pamoja kwa maslahi ya
nchi.
‘’Kwa mfano, kule Mvomero tulianzisha mpango wa
kupima ardhi, mpango bora wa matumizi ya ardhi, lakini baadae kutokana na
mwingiliano wa sheria, vikaundwa vijiji ndani ya vijiji,’’ alisema.
Alisema katika maeneo ambayo tayari wananchi
walishapatiwa hati, halafu inadaiwa ni hifadhi za mazingira, ni dhahiri wizara
hizo mbili zinapaswa kuangalia njia bora ya kuodokana na mgogoro huo.
Aliwataka wananchi wa Mkundi katika Manispaa ya
Morogoro waliovunjia nyumba zao kwa madai wamevamia eneo la hifadhi, kuvuta
subira huku serikali ikifuatilia kuona usahihi wa jambo hilo.
No comments:
Post a Comment