Wednesday, 20 January 2016

ASKARI KIZIMBANI KWA KUMBAKA MWANAFUNZI




ASKARI Polisi wa Kikosi cha Kuzuia na Kutuliza Ghasia (FFU), Rafael Makongojo, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arumeru, kujibu tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Wasichana ya Korogwe.
Makongojo, alifikishwa katika mahakama hiyo jana,  saa 4:40, asubuhi na kusomewa shitaka hilo na Wakili wa Serikali, Sabina Silayo, mbele ya Hakimu Jasmin Abdul.
Silayo alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Jumamosi iliyopita, eneo la kwa Mrombo, karibu na kilipo kikosi cha FFU.
Mshitakiwa alikana shitaka hilo, ambapo Wakili Sabina alidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu alikubaliana na ombi hilo, hivyo aliahirisha shauri hilo hadi Januari 25, mwaka huu, kwa usikilizwaji wa awali.
NJE YA MAHAKAMA
Wakati mtuhumiwa huyo akitolewa rumande kwa ajili ya kupelekwa mahakamani, askari polisi waliomleta waliwazuia waandishi wa habari kuingia katika chumba cha mahakama.
Mbali na kuwazuia waandishi hao, askari walikuwa wakiwatolea lugha chafu licha ya kuwa na kibali kutoka kwa hakimu anayesimamia mahakama hiyo.
Wakati mtuhumiwa akiingizwa mahakamani, polisi walikuwa wanamzonga kisha kuwataka waandishi wa habari watoke nje kwani hawakutaka apigwe picha.
Hata hivyo, waandishi wa habari waligoma na kuendela kuzozana na polisi waliokuwa mlangoni, wakilazimisha kuingia wakati shauri hilo likiendelea.
ABEBEWA NA GARI MAALUMU
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mtuhumiwa huyo baada ya kusomewa shitaka hilo, alipitishwa mlango wa uani na askari polisi na kurudishwa mahabusu kwa lengo la kuwakwepa waandishi wa habari.
Hata hivyo, wakati mahabusu wakiondolewa katika mahakama hiyo kupelekwa gereza la Kisongo, Rafael alibebwa na gari aina ya Land Cruiser, lenye namba za usajili T 866 BGB, badala ya basi la magereza, ambalo lilibeba watuhumiwa wote waliokuwa mahakamani hapo.

No comments:

Post a Comment