VIGOGO wa Halmashauri ya Mji wa Kahama
mkoani Shinyanga, wamengia kitanzini kutokana na upotevu wa fedha zinazotolewa
na kampuni ya ACACIA inayoendesha mgodi wa Buzwagi.
Fedha hizo ni zile zinazotolewa kwa
halmashauri kila baada ya robo ya mwaka kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa
Kahama, Abel Shija, alisema jana kuwa, hatua hiyo inatokana na taarifa ya
uchunguzi iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya, Vita Kawawa.
Alisema taarifa hiyo ilililazimu
Baraza la Madiwani kukutana kuijadili pamoja na kuchukua hatua dhidi ya
watendaji na watumishi wanaohusika na kashfa hiyo.
Alisema watumishi watano
wamesimamishwa kazi, ambao ni Wilfred Kishere (Mweka Hazina), Alex Mroso (Mhasibu), Michael Nzingula (Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini) na Katibu wake, Joseph Maziku pamoja na Elius Mollel, ambaye ni Ofisa
Biashara.
Hata hivyo, alisema kuna watumishi
wengine watano wanaoguswa na kashfa hiyo na kwamba, wataendelea na kazi wakati
uchunguzi dhidi yao ukiendelea.
Aliwataja watumishi hao kuwa ni Anastazia
Manumbu, Joakim Henjewele, Kulwa S.N, Neema Lema na Angela Clavel.
Aliongeza kuwa tayari aliyekuwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Felix Kimaryo na Msumba Msoka, aliyekuwa Mhandisi,
wameshahamishwa vituo vya kazi.
Hata hivyo, alisema anaamini
kuhamishwa kwa watendaji hao kumelenga kuwalinda ili wasijibu tuhuma
zinazowakabili na kwamba, watapambana kuhakikisha wanarudi kuzijibu.
“Tuna imani idara ya utumishi
itawarejesha hapa kujibu tuhuma zinazowakabili. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) inaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na hili,” alisema.
No comments:
Post a Comment