Wednesday, 20 January 2016

TTCL KUMILIKIWA NA SERIKALI KWA ASILIMIA 100





BAADA ya malalamiko ya muda mrefu kuhusiana na mwenendo wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), iliyoingia ubia na Bhart Airtel, hatimaye serikali imetangaza kuirejesha chini ya umiliki wake kwa asilimia 100.
Tangu kampuni hiyo kubinafsishwa, wadau walikuwa wakipaza sauti kutokana na ufanisi mdogo, ikiwemo kutokwenda na kasi ya mabadiliko huku mshirika wake akipiga hatua kwa kasi.
Kutokana na malalamiko hayo na sababu zingine mbalimbali, serikali imesema ipo katika hatua za mwisho za kuilipa Bhart Airtel ili kurejesha umiliki wa asilimia 100 katika TTCL. 
Uamuzi huo umepangwa kutekelezwa kabla ya mwisho wa mwezi huu, ambapo utaiwezesha TTCL kurejesha hisa zake asilimia 35 zilizonunuliwa na Airel mwaka 2001.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alitangaza uamuzi huo jana, mkoani Mtwara, alipotembelea ofisi za TTCL, kukagua mitambo na miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
"Serikali imesikia kilio cha muda mrefu cha Watanzania na wadau wote wa TTCL kuhusu kuondoka kwa mbia mwenza Bhart Airtel. Ubia huu wa TTCL na Bhart Airtel utahitimishwa rasmi kabla ya mwisho wa mwezi huu.
“Tumefanya majadiliano ya kutosha na kukubaliana kuwa serikali iilipe Bhart Airtel sh. bilioni 14.9 ili kurejesha hisa asilimia 35 ndani ya TTCL na kuifanya kuwa mali ya umma kwa asilimia 100.
"Tutatumia fedha za mapato ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kukamilisha utaratibu huu. Naiagiza bodi na menejimenti ya TTCL kufanya kazi kwa bidii na ufanisi mkubwa na kusimamia kikamilifu shughuli za TTCL ili kutimiza jukumu lake kwa umma," alisema Profesa Mbarawa.
Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Profesa Tolly Mbwette, alisema kukamilika kwa mchakato huo ni hatua muhimu kwa uhai na ufanisi wa TTCL na kusisitiza mpango wa mageuzi ya kibiashara wa kampuni hiyo, ambao sasa utatekelezeka kwa kasi kubwa baada ya hatua hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura, alisema jitihada kubwa za TTCL sasa zitaelekezwa katika kuboresha huduma kwa kutumia fedha za ndani na mikopo ya wadau wa kibiashara, ili kuiwezesha TTCL kuendelea kuwa kiongozi katika utoaji wa huduma bora na nafuu katika soko la mawasiliano nchini.
Aidha, TTCL na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), zimeingia makubaliano ya mkopo wa fedha na dhamana za benki utakaoiwezesha TTCL kupata Dola za Marekali milioni 329 (sh. bilioni 15.08) ili kuingiza mitambo mipya ya kisasa itakayoboresha huduma zake, ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma za miamala ya fedha kwa njia ya mtandao.

WASOMI WAPONGEZA
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, Tawi la Dar es Salaam,Eston Ngilangwa, alisema maamuzi hayo ya serikali ni hatua muhimu ya kufufua kampuni hiyo iliyokuwa ikijiendesha kwa hasara.
Alisema endapo serikali itafanikisha mchakato huo, wananchi watapata nafuu zaidi kwenye huduma ya mawasiliano kwa kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu.
Hata hivyo, alionya kuwa serikali inapaswa kuweka mikakati thabiti ya kuisimamia kampuni hiyo ili kutorudia makosa yaliyosababisha kudorora.
Naye Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Mhandisi Peter Chisawilo, alisema wazo la kuuza asilimia 35 ya hisa za TTCL kwa Airtel lilikuwa baya.
Alisema wananchi wengi walishangazwa na hatua hiyo, ambayo ilisababisha uwepo wa kampuni nyingi za simu nchini kutoka nje ya nchi, zilizochangia kuzorota kwa huduma za TTCL ambazo zilianza kuonyesha matumaini.
Mhandisi huyo alisema kutokana na serikali kushindwa kuwa na maamuzi ya asilimia 100 kwenye kampuni ya TTCL, kulisababisha kukwama kwa mambo mengi katika sekta ya mawasiliano, ambayo kutokana na uwepo wa mkongo wa taifa, yangefanyika kikamilifu.
“Kumegua umiliki wa TTCL kuliiacha nchi katika hali mbaya ya kuangalia wageni wakihodhi sekta ya mawasiliano, ambapo walikuwa wakijiamulia viwango vya huduma ili kujipatia faida huku wakimkamua mtanzania,” alisema.
Alisema umiliki wa asilimia 100 wa kampuni hiyo unaokusudiwa kufanywa na serikali ndani ya wiki moja kuanzia sasa, yatakuwa mapinduzi mapya ya sekta ya mawasiliano na kutakuwa na unafuu mkubwa kwenye huduma za mawasiliano, hivyo uchumi utakuwa kwa kasi.
Aidha, Mhandisi huyo alisema serikali inatakiwa kuwashurutisha wamiliki wa kampuni za simu kuuza hisa zao kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ili kuwe na uwazi wa mapato ya kampuni hizo na pia wananchi waweze kumiliki sehemu ya kampuni husika.
Kuhusu TTCL, alisema mara itakapomilikiwa kwa asilimia 100 na serikali siku chache zijazo, serikali iangalie uwezekano wa kutoa baadhi ya umiliki wa hisa kama ilivyofanya kwa Benki ya NMB.

No comments:

Post a Comment