Thursday, 21 January 2016
CCM YAPATA PIGO, MAKAMU MWENYEKITI UWT AFARIKI, DK. MAGUFULI AMTUMIA SALAMU ZA RAMBIRAMBI JK
MAKAMU Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake Tanzania (UWT), Asha Bakari Makame, amefariki dunia nchini Dubai alikokuwa amekwenda kwa mapumziko baada ya kutoka kwenye matibabu.
Asha, ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.
Tayari Rais Dk. John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete, kutokana na msiba huo mkubwa kwa Chama.
Taarifa ya CCM iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, jana, imesema kuwa mwili wa marehemu utawasili visiwani Zanzibar leo. Aidha, imesema kuwa taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa, ambapo marehemu atazikwa kesho saa 4:00 asubuhi Zanzibar.
CCM imesema kifo cha Asha kimeacha pigo kubwa kwa kuwa alikuwa kiongozi na mwanachama makini na aliyekuwa mstari wa mbele katika kukijenga Chama, hivyo mchango wake utaendelea kukumbukwa daima.
Katika salamu zake za pole kwa Rais mstaafu Kikwete, Dk. Magufuli amemuelezea Asha kuwa alikuwa kiongozi hodari, mchapakazi na aliyeipigania nchi yake, hususani Muungano.
Dk. Magufuli alimuomba Kikwete, kumfikishia salamu za pole kwa viongozi wa Chama na serikali ya Zanzibar, wana CCM, ndugu na jamaa wote wa marehemu walioguswa na msiba huo mkubwa.
"Nimesikitishwa sana na kifo cha Asha na ninamwombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, amina," alisema Rais Magufuli.
Mbali na Asha, CCM pia imepata pigo lingine kutokana na kifo cha Mwenyekiti wa CCM Tawi la DMV huko Maryland nchini Marekani, George Sebo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mazishi ya Sebo yatafanyika Januari 30, mwaka huu, katika Mji wa Maryland nchini humo.
Zanzibar ni shwari
Katika hatua nyingine, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, amemweleza Dk. Magufuli kuwa hali ni shwari huku amani na utulivu vikiendelea kutawala.
Balozi Iddi alikutana na Dk. Magufuli, Ikulu mjini Dar es Salaam, jana, ambapo alisema hali ni tofauti na inavyoripotiwa kwenye vyombo vya habari kuwa si shwari.
“Zanzibar ipo salama, yenye amani na tulivu, nimechukua hatua ya kuja kumjulisha Rais Magufuli kwa kuwa yeye ni kiongozi wetu.
"Hayo yanayoandikwa kwenye magazeti kuwa Zanzibar kuna fujo, mara kutatokea machafuko… sio kweli, kama unavyojua uchaguzi ulifutwa na tume ya uchaguzi na tunasubiri tarehe mpya ya uchaguzi itangazwe ili tufanye uchaguzi," alisema Balozi Iddi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment