Monday, 4 January 2016

PROFESA MBARAWA AWASHA MOTO TRL


SEHEMU ya tuta la reli lililosombwa na maji kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha eneo la Magulu.


WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akipanda kiberenge cha TRL baada ya kukagua eneo la reli lililoathiriwa kwa mvua.



NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewataka watendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (RAHCO), kuhakikisha sehemu ya reli iliyosombwa na mafuriko wilayani Kilosa mkoani Morogoro, inaunganishwa ndani ya siku tatu na huduma za treni kurejea.
Profesa Mbarawa alisema hayo jana, baada ya kukagua sehemu ya reli hiyo kutoka Kilosa hadi Magulu- Kidete ili kuona athari zilizosababishwa na mafuriko yaliyotokana na mvua zilizonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma.
“Fanyeni kazi usiku na mchana ili ikifika Alhamisi ya wiki hii, mawasiliano ya reli kati ya mkoa wa Morogoro na Dodoma yawe yamerejea na abiria waendelee kupata huduma ya treni,” alisema.
Aliwataka wananchi wa vijiji vya Munisagara, Mkadage,  Mzaganza, Magulu na Kidete kutoa ushirikiano kwa serikali ili ukarabati wa ujenzi wa reli hiyo ukamilike kwa haraka.
Profesa Mbarawa aliwataka wananchi waishio pembezoni mwa reli katika wilaya ya Kilosa, kupanda miti ili kuzuia mmomonyoko wa udongo unaosababisha mafuriko kwa urahisi wakati wa mvua na kubomoa reli kila wakati.
“Pandeni miti, lindeni miundombinu ya reli na acheni vitendo vya  uharibifu wa mazingira ili ujenzi wa mwaka huu uwe wa kudumu na reli isiathiriwe kirahisi na kuwasababishia kero wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kidete, Mohamed Mbunda, alisema wananchi watashirikiana na serikali kulinda mazingira ili kudhibiti mafuriko yanayoharibu miundombinu ya reli kila wakati wilayani humo.
Mafuriko wilayani Kilosa ni matokeo ya mvua zinazonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma, ambazo husababisha maji ya Mto Mkondoa kuacha mkondo wake na kubomoa tuta la reli katika eneo la Msagali hadi Kilosa kila wakati.
Mvua za hivi karibuni zilizonyesha mkoani Iringa na Dodoma, zimesomba reli katika eneo la Magulu—Kidete, umbali wa kilomita 315 kutoka Dar es Salaam na kukata mawasiliano ya reli kwa siku tatu sasa.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa aliwataka watendaji wa TRL na RAHCO kutafuta suluhisho la kudumu katika madaraja 32 yaliyo katika mtandao wa reli ya kati ili yasiathiriwe na mvua wakati wote.

No comments:

Post a Comment