Monday, 4 January 2016
WASIOENDELEZA VITALU VYA MADINI KUNYANG'ANYWA
Na Mwandishi Wetu, Singida
SERIKALI imesema itawanyang’anya vitalu vya madini visivyoendelezwa na kuwapatia wachimbaji wadogo nchini ili waviendeleze.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, alisema hayo jana, wakati akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Fatma Toufiq, kabla ya kukagua miradi ya uchimbaji madini ya umeme wilayani humo.
“Tutachukua maeneo yasiyoendelezwa na kuwagawia wachimbaji wadogo kama Sheria ya Madini ya mwaka 2010, inavyoelekeza, hivyo Kamismhna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati hakikisha hilo linatekelezwa,’’ alisema.
Dk. Kalemani alisema hayo baada ya Fatma kumueleza changamoto wanazokumbana nazo wachimbaji wadogo katika wilaya hiyo, ikiwemo utumiaji wa zana duni za uchimbaji madini na ukosefu wa maeneo ya uchimbaji kutokana na watu kuhodhi maeneo hayo kwa muda mrefu bila kuyafanyia kazi.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya alisema pamoja na changamoto za wachimbaji wadogo, wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya umeme kukatika mara kwa mara, hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi za wananchi katika wilaya hiyo.
Hata hivyo, Dk. Kalemani alisema umeme katika wilaya hiyo na mikoa ya Iringa, Singida, Dodoma na Kanda ya Ziwa, utatengemaa baada ya ujenzi wa njia kuu ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga, kukamilika Juni, mwaka huu.
Alisema mitambo hiyo itasafirisha umeme kwa kiwango kikubwa, tofauti na miundombinu ya sasa, ambayo inasafirisha umeme kwa msongo wa kilovoti 220.
Naibu waziri huyo aliwataka watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), katika wilaya hiyo kuhakikisha umeme haukatiki kwa sababu ya uzembe wa kibinadamu.
“Watendaji wa TANESCO nileteeni taarifa kwa nini umeme unakatika mara kwa mara katika wilaya hii na kama ni uzembe wa mtu, basi naye akatike hapo hapo,” alisema.
Wakati huo huo, Dk. Kalemani ameitaka Kampuni ya Spencon, iliyopewa tenda ya kusambaza umeme katika vijiji 90 mkoani Singida, kukamilisha kazi hiyo ifikapo Mei, mwaka huu.
Alitoa agizo hilo baada ya kampuni hiyo kusuasua katika kusambaza umeme vijijini kwani kazi ya kusambaza umeme katika vijiji hivyo ilipaswa kukamilika Novemba, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment