Thursday, 21 January 2016
RAIS MAGUFULI AMSIMAMISHA KAZI KAMISHNA WA IDARA YA UHAMIAJI
RAIS Dk. John Magufuli amewasimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Idara ya Uhamiaji nchini, Sylvester Ambokile na Kamishna anayeshughulikia Utawala na Fedha, Piniel Mgonja.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana, imeeleza kuwa makamishna hao wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, kufuatia dosari alizozibaini Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, wakati wa ziara yake ya kazi katika idara hiyo hivi karibuni.
Taarifa hiyo iliyomnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, ilisema dosari hizo ni tuhuma za rushwa, ukusanyaji mbaya wa maduhuli ya serikali, ukiukwaji wa taratibu za manunuzi na utendaji mbovu.
Balozi Sefue amesema watendaji hao wakuu wa Uhamiaji wamesimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika.
Wakati huo huo,Rais Magufuli amemrejesha Eliakim Maswi kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Manyara, baada ya kukamilisha kazi maalumu aliyomtuma kuifanya katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kabla ya kurejeshwa Manyara, Maswi aliteuliwa kuwa Kaimu Naibu Kamishna TRA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment