Friday, 29 January 2016

TUMBUA MAJIPU YA JPM YAWATISHA UKAWA




WABUNGE wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wameanza kuweweseka kutokana na kasi ya utumbauji majipu, inayofanywa na serikali ya awamu ya tano, ambapo wamedai kuwa kasi hiyo ni kubwa na haizingatii taratibu.

Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Fremaan Mbowe, alisema hayo juzi, bungeni mjini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari. Mbowe alisema hivi sasa kumekuwa na kasi kubwa ya kutumbua majipu, inayofanywa na serikali ya awamu ya tano, lakini ni vyema kasi hiyo ikawa inafuata taratibu na ubinadamu.

“Tunasema kutumbua majipu, lakini ni lazima tujue tunatumbua kwa kutumia kitu gani, mikasi au jiwe lenye ncha kali, lakini pia tuangalie huyo anayetumbuliwa ana familia na kuna watu wanaomtegemea,’’ alisema.

Alisema hawataki serikali ifuge uzembe, lakini kama sheria zinazotumika kutumbua majipu ni mbovu ama zimepitwa na wakati, ni vyema zikarudishwa bungeni ili zifanyiwe marekebisho. 


“Tunaona kuwa utaratibu wa sasa wa kutumbua majipu hauzingatia hata haki za kibinadamu. Balozi yuko Tokyo, anapigiwa simu siku hiyo hiyo apande ndege arudi Tanzania, bila kujali kuwa ana watoto, familia sasa unapomwambia arudi siku hiyo, hujamtendea haki,” alisema. 

Aliongeza:“Ikiwa kanuni, taratibu na sheria zinazotumika kuwawajibisha watendaji wazembe haziendani na wakati, zirudishwe bungeni zifanyiwe marekebisho.”

Mbowe alisema kila jambo ni vyema likafanyika kwa taratibu na kwamba waliihukumu serikali ya awamu ya nne kwa kushiriki uovu.

Aliiomba serikali kuzingatia haki, kanuni, taratibu na sheria za utumishi wakati inapotumbua majipu ili isije ikaingia kwenye mgogoro wa kisheria.

ULINZI WAIMARISHWA BUNGENI

SIKU moja baada ya wabunge wa upinzani kufanya vurugu na kulazimika kutolewa nje chini ya ulinzi mkali wa polisi, ulinzi mkali

umeimarishwa eneo la viwanja vya bunge. Uhuru, ilishuhudia askari wakiwemo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakiwa wametanda kila kona ya eneo la bunge kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, ikiwemo lango la kuingilia bungeni.

Askari hao walikuwa wamejipanga vyema kwa ajili ya kudhibiti hali yoyote ambayo ingeweza kujitokeza. Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu, jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema vurugu zilizotokea juzi hakuna aliyeshikiliwa.

Hata hivyo, alipotakiwa kuelezea kuhusu tukio la juzi, alijibu kwa ufupi kuwa hana maelezo ya zaida na hakuna anayeshikiliwa.

 UKAWA WAENDELEZA VURUGU BUNGENI

Vitendo vya zomea zomea na kutoka ndani ya bunge, vinavyofanywa na baadhi ya wabunge wa upinzani, vimeendelea tena jana, baada ya wabunge wote wa upinzani kutoka nje. Hatua hiyo ilitokana na kukataliwa miongozo yao na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson.

Dk. Tulia alichukua uamuzi huo, baada ya mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko (CHADEMA), kuomba mwongozo na kudai kuwa Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa alilidanganya bunge kwa kudai elimu ni bure wakati kuna baadhi ya shule zinachangishwa magunia kwa maguni ya vyakula. 


Kutokana na mwongozo huo, Dk. Tulia alitoa ufafanuzi kuwa suala la elimu bure limeshatolewa ufafanuzi na Waziri wa Nchi, Ofi si ya Rais-TAMISEMI, George Simbachawene, lakini kuna changamoto zake ambazo serikali inazifanyiakazi.

Baada ya ufafanuzi huo, Ester alikaa chini, lakini wabunge wenzake walitaka majibu ya mwongozo huo yatolewe na waziri husika. Wakati wakidai hayo, wabunge wengi wa upinzani walisimama na kutaka kutoa miongozo, ndipo Dk. Tulia alipowakatalia na kuamua kutoka nje wote. Wakati wakitoka nje ya ukumbi wa bunge, walisikika wakiwarushia maneno ya ‘vijembe’ askari waliokuwa wakilinda hali ya usalama.

Katika mwongozo wa Ester, alisema wakati Waziri Mkuu akijibu swali la Paulin Gekul, alieleza kuwa serikali ilikuwa ikichukua ada ya sh. 70,000, kwa shule za bweni na sh. 20,000, kwa shule za kutwa. Alisema katika majibu hayo, Waziri Mkuu atakuwa ama amebahatisha au hajapata maelezo ya kutosha kuhusu shule za bweni, akitoa mfano wa moja ya shule ambayo watoto wanalipishwa gharama za vyakula.

“Kwa  nini Waziri Mkuu anatoa maelezo asiyo na uhakika wakati watoto bado wanaambiwa waende na chakula shule,” alisema. 


Baada ya kutoa maelezo hayo, Dk. Tulia alisema: ”Itakumbukwa Waziri wa TAMISEMI, vikao vilipoanza, alitoa maelezo kuwa huo ni mwanzo na zipo changamoto ambazo wizara inazifanyia kazi.” 

Aliongeza: “Hayo maelezo amekuwa akiyatoa mara kwa mara, elimu ni bure, lakini bado ziko changamoto.” 

Maelezo hayo ya Dk. Tulia yaliwafanya baadhi ya wabunge wa upinzania kuanza kuzomeazomea. 

“Mheshimiwa Lema unazijua taratibu, umeomba mwongozo ndiyo ninaotoa, maelezo ninayotoa ndio mwongozo,”alisema Naibu Spika huku kelele za kuomba mwongozo zikiendelea kusikika. Kabla ya Naibu Spika kukaa kwenye kiti chake, wabunge hao wa upinzani walisimama na kuamua kutoka nje ya ukumbi wa bunge.

No comments:

Post a Comment