WAZIRI wa Katiba na Sheria Dk. Harrison Mwakyembe,
ameuagiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kusitisha mara moja
usajili mpya wa wadhamini wa asasi, vyama, misikiti na vikundi mbalimbali vya
kijamii.
Amesema amefikia uamuzi huo kwa lengo la kufanya uhakiki
wa uhalali wa kuwepo kwa taasisi hizo kisheria.
Pia, ameagiza kuwa uhakiki huo ukamilike ndani ya
miezi mitatu (siku 90), kuanzia sasa na orodha kamili ya wadhamini ikiwa ni
pamoja na picha zao, anuani za posta na makazi na taarifa nyingine muhimu za
utambuzi wa taasisi hizo mahali zilipo.
Alisema taarifa hizo ziwasilishwe RITA na nakala
zipelekwe wizarani kwa uhakiki na kumbukumbu.
Waziri Mwakyembe alitoa agizo hilo jana,
alipokutana na watendaji na uongozi wa Bodi ya RITA, kwa lengo la kuboresha utendaji
wa wakala, lengo likiwa kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano.
RITA ina zaidi ya wadhamini 5,000, walio kwenye
vitabu vyao vya usajili.
Wakati huo huo, Waziri Dk. Mwakyembe ameitisha
kikao wiki ijayo cha mamlaka zote zinazohusika na usajili wa vikundi vya kijamii,
mashirika, kampuni na asasi mbalimbali.
Alisema lengo la kikao hicho ni kuimarisha
taratibu za usajili na uendeshaji na kuboresha mawasiliano baina ya vyombo vya
usajili vya dola ili kulinda maslahi mapana ya taifa.
No comments:
Post a Comment