RUNGU la tumbua tumbua majipu la serikali ya awamu
ya tano limehamia Wizara ya Maliasili na Utalii, ambako watendaji wakuu,
wakiwemo wakurugenzi wa Idara ya misitu na wanyamapori wameangukiwa na rungu
hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya rungu hilo kutembea
kwenye wizara na idara kadhaa, tangu serikali ilipoanza kazi rasmi, Novemba 5, mwaka
jana na kusababisha utendaji wenye kuzingatia weledi na maadili ya utumishi wa
umma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne
Maghembe, jana alitangaza kuwasimamisha
kazi Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Huduma za Misitu Nchini (TFS), Juma Mgoo na wakurugenzi
wawili wa wakala huo.
Wakurugenzi hao ni Zawadi Mbwambo, ambaye alikuwa Mkurugenzi
Rasilimali Misitu na Kaimu Mkurugenzi wa
Mipango, Matumizi na Uendelezaji wa Misitu, Nurdin Chamuya, ambao wamesimamishwa
kazi kupisha uchunguzi kutokana na
ukusanyaji usioridhisha wa mapato yatokanayo na mazao ya misitu.
Aidha, rungu hilo limewaangukia wakuu wa kanda za wakala
wa huduma za misitu nchi nzima, ambao ni Hubert Haule wa Kanda ya Kusini na Bakari Rashidi wa Kanda ya Mashariki.
Wengine ni Shabani Mwinyi Juma wa Kanda ya Kati,
Emmanuel Minja wa Kanda ya Magharibi na Bruno Mallya wa Nyanda za Juu Kusini, ambao wamesimamishwa
kutokana na kuwepo wa mapato yasiyoridhisha katika idara hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa
Matumizi Endelevu, Dk. Charles Mulokozi, pia amesimamishwa kazi kwa kosa la
kukaidi agizo la kutosaini vibali vya kusafirisha wanyamapori nje ya nchi.
Alisema amechukua hatua hiyo baada ya juzi, nyani
61, kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na
kubainika kuwa, Idara ya Wanyamapori ilitoa kibali cha kusafirisha nyani hao,
kikiwa kimetiwa saini na mkurugenzi huyo.
Waziri Maghembe alisema ndege kutoka Ulaya
iliyotakiwa kusafirisha nyani hao, imeshikiliwa pamoja na rubani wake kwa ajili
ya kuhojiwa.
Taarifa zaidi zilizopatikana zimeeleza kuwa nyani
450, ndio waliokuwa wanawindwa kwa ajili ya kusafirishwa.
Katika kikao chake na waaandishi wa habari,
Profesa Maghembe alifafanua zaidi kuwa kwa upande wa Idara ya Misitu, alibaini fedha
zitokanazo na makusanyo ya mazao ya misitu zimekuwa hazipelekwi benki kwa
wakati na hata zikipelekwa, huwa pungufu na kile kilichokusanywa.
Alisema siku chache zilizopita alipata taarifa
zilizobainisha kuwa, shehena kubwa ya magogo ya miti aina ya mninga mkoani
Rukwa, yalikatwa na kuwekwa ndani ya makontena msituni.
Alisema magogo hayo pia yalikuwa yametengenezewa
nyaraka bandia zinazodaiwa kutoka Zambia, ambazo zilifanya maandalizi ya
kusafirishwa kupelekwa China kukamilika.
Waziri Maghembe alisema licha ya magogo hayo
kubainika, Wakala wa Misitu haukuchukua hatua yoyote kwa watuhumiwa ili
kuonyesha kujali rasilimali za taifa.
Alisema baada ya kubaini hivyo, kulifanyika hila
ambapo usiku wa jana, alipata taarifa kuwa
shehena ya magogo hayo yenye thamani
ya sh. milioni 500, badala ya
kupelekwa makao makuu ya wilaya ya Kalambo, yalimwagiwa petroli na kuchomwa moto.
No comments:
Post a Comment