Sunday, 27 March 2016

DK. SHEIN AAPISHWA. AAHIDI KUTEUA VIONGOZI MAKINI NA WAADILIFU




RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amesema ataunda serikali makini yenye viongozi waadilifu na wachapa kazi, ambao watatenda haki kwa wananchi wa Zanzibar.

Pia, amesema atahakikisha anaimarisha ulinzi wa nchi na hatakubali mtu au kikundi cha watu kuleta vurugu na kuhatarisha amani ya Zanzibar.

Dk. Shein, alitoa kauli hiyo jana, muda mfupi baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa awamu ya saba.

Sherehe za kuapishwa Dk. Shein, zilifanyika kwenye Uwanja wa Amaan na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Pia, viongozi mbalimbali wa serikali na wageni mashuhuri  walihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Dk. Shein, aliyeshinda
kwa kishindo katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

Katika hotuba yake aliyoanza kuitoa saa 5:54 asubuhi hadi saa 6:17 mchana, Dk. Shein, alisema ataunda serikali makini kwa kufuata nyayo za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli.

Dk. Shein alisema serikali yake itaendeleza kaulimbiu ya Rais Magufuli ya 'Hapa Kazi Tu' na itakuwa makini kwa kutenda
haki kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Alisema anataka kuunda serikali, ambayo itakuwa na ustawi mzuri kwa wananchi wa Tanzania, lakini hatakubali mtu au
kikundi cha watu kuanzisha vurugu.

Dk. Shein alisema serikali yake itakuwa na mtazamo chanya wa kuwahudumia wananchi wa Zanzibar bila kujali itikadi za
vyama.

"Leo sio siku ya kutoa hotuba, nitaitoa baada ya kutangaza baraza la tisa la wawakilishi muda mfupi ujao, lakini napenda kuwaahidi itakuwa makini yenye kutenda haki bila kujali itikadi za kisiasa," alisema Dk. Shein.

Alisema atatumia uzoefu wa miaka mitano aliyokuwa madarakani, kufanyakazi kwa weledi, akifuata Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015.

Dk. Shein alisema atashirikiana na vyama vya upinzani kuwaletea wananchi wa Zanzibar mafanikio na amepokea ushauri wa aliyekuwa mgombea wa ADC, Hamad Mohammed Rashid.

Katika hotuba fupi aliyotoa wakati wa kutangaza matokeo kwenye ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani, Machi 21, mwaka huu, Rashid alimuomba Dk. Shien kutumia usomi na utendaji wake bora wa kazi, kutatua kero za Wazanzibari ikiwemo mpasuko wa kisiasa.

Dk. Shein alidokeza kuwa uchaguzi umemalizika na alitoa rai kwa wananchi wa Zanzibar kurejea katika shughuli za kawaida
za ujenzi wa taifa.

"Uchaguzi umemalizika, naomba wananchi wote kwa ujumla wenu, kurejea katika kazi za ujenzi wa taifa. Nchi itakuwa katika
hali ya amani na utulivu, msiwe na wasiwasi," aliongeza Dk. Shein.

Aliwapongeza wanachama wa CCM na wananchi wa Zanzibar kwa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu. Pia, alivipongeza vyombo vya ulinzi kwa kufanya kazi kwa weledi.

Aidha, aliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), iliyokuwa chini ya Mwenyekiti, Jecha Salim Jecha, aliyekuwa kivutio uwanjani hapo.

Wananchi waliohudhuria sherehe hizo mara kwa mara waliimba nyimbo za kumsifu Jecha na hata picha yake ilipochomoza katika kamera ya uwanjani, walilipuka kwa shangwe.

Awali, Dk. Shein, aliwasili kwenye Uwanja wa Amaan, saa 4:40 asubuhi, akiwa katika msafara maalumu wa pikipiki na magari na kulakiwa na maelfu ya wananchi.

Baada ya kuwasili uwanjani hapo, Dk. Shein, alikwenda moja kwa moja katika kibanda maalumu alichoandaliwa kwa ajili ya
kupigiwa wimbo wa taifa na mizinga 21.

Dk. Shein, alianza kukagua gwaride saa 4:47 asubuhi na bendera ya Rais ilishushwa saa 4:56, kuashiria ukomo wa serikali yake kabla ya kupandishwa mpya baada ya kula kiapo.

Dk. Shein alikula kiapo saa 11:00, mbele ya Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omari Othumani Makungu, viongozi wa dini na baadaye kukagua tena gwaride na kupigiwa mizinga 21.

Viongozi wa dini waliotoa hotuba za kumtakia kila la kheri ni Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ali Khamis, Askofu Madhehebu ya Katoliki, Augustino Shayo na Mkuu wa Maaskofu wa Anglikana, Michael Henry.

Mbali na Rais Magufuli, viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana.

Wengine ni Makamu wa Rais mstaafu Dk. Mohammed Gharib Bilal, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amaan Abeid Karume, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, January Makamba, Waziri wa Utumishi, Angela Kairuki na Waziri wa Mambo wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.

Pia, walikuwepo Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai, Naibu Spika, Dk. Tulia Mwansasu, Jaji Mkuu wa Tanzania Bara, Othuman Chande, Jaji Augustino Ramadhani na Waziri Kiongozi wa zamani wa Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha.

Jecha, alimtangaza Dk. Shein kuwa Rais Mteule wa Zanzibar, baada ya kupata kura 299,982, sawa na asilimia 91.4, kati ya kura 341,865 zilizopigwa.

Katika uchaguzi huo uliokuwa wa amani na utulivu, idadi ya wapiga ilikuwa 503,580 na kura zilizoharibika ni 13,327. Jumla ya vyama 14 vilishiriki.

No comments:

Post a Comment