Tuesday 1 March 2016

NGONYANI AZITAKA TAASISI KWENDA NA KASI YA MAGUFULI



NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kufanyakazi kwa uadilifu, bidii na kwa uharaka ili kuendana na kasi ya madiliko ya serikali ya awamu ya tano.
Alisema hayo jana, mjini Dar  es Salaam, wakati alipofanya ziara katika taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ikiwemo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kwa lengo la kupata mafunzo ya kiutendaji katika taasisi hizo.
Aidha, alizitaka taasisi hizo kuongeza ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vya mapato walivyonavyo, badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
“Nataka ifikapo mwaka wa fedha ujao, makusanyo ya mapato yawe yameongezeka zaidi kuliko matumizi na kamwe msikae kusubiri ruzuku kutoka serikalini, kikubwa ni kubuni vyanzo vyengine vya mapato ili kuweza kujiendesha”, alisema.
Hata  hivyo, naibu waziri huyo aliwataka watendaji wa taasisi hizo kufanyakazi kwa weledi na bila woga kwani serikali haitamuonea huruma yeyote anayekiuka kutekeleza wajibu wake.
“Nawaomba mfanyekazi kwa morali kubwa ili kuisaidia jamii, ambayo inahitaji huduma muhimu kutoka serikalini,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Ngonyani alimtaka Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Manase Ole Kujan, kutatua changamoto walizonazo ili kuleta mabadiliko chanya katika taasisi hiyo.
“Unayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko hasa katika mfumo mzima wa ukatishaji tiketi eneo la Magogoni, ambalo limekuwa kero katika mfumo mzima wa ukusanyaji wa mapato,” alisisitiza.
Mbali na hilo, alimtaka Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, kuandaa taarifa ambayo itaonyesha idadi ya nyumba za serikali wanazomiliki na ibainishe taarifa ya watumishi wenye stahili ya kupangishwa kwenye nyumba hizo.
Kwa upande wake, Mhandisi Ole Kujan alisema wakala huo umepanga kuboresha miundombinu, hasa katika usafiri wa majini na kuhakikisha inapunguza  changamoto ya usafiri katika vivuko.
Naye Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa baraza la taifa la ujenzi, Mhandisi Julius Mamilo, alieleza changamoto walizonazo, ikiwemo uhaba wa fedha, hali inayosababisha baraza hilo kukwama katika kufanya kazi katika miradi yake ya maendeleo, hususan kazi za utafiti.

No comments:

Post a Comment