MAMLAKA
ya Mapato Tanzania (TRA), imetangaza kufuta msamaha wa kodi kwa wafanyabiashara
wanaoingiza bidhaa kutoka nchini China.
Awali,
TRA iliweka kodi elekezi kwa bidhaa kutoka China, ambapo sasa wafanyabiashara
watatakiwa kulipa kulipa kodi halisi inayotakiwa ili kuweka uwiano sawa na
bidhaa zingine zinazoingizwa nchini.
Pia,
TRA imetangaza kukusanya mapato ya sh. trilioni 8.6, ikiwa ni asilimia 99 ya
malengo iliyojiwekea kwa mwezi Februari, mwaka huu, na kwamba itaongeza kasi
zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Kaimu
Kamishina wa TRA, Alphayo Kidata, alisema jijini Dar es Salaam, jana, kuwa serikali
kupitia mamlaka hiyo, imefuta kodi elekezi hiyo, ambayo ilikuwa ikiwapa punguzo
la kodi wafanyabiashara wanaoagiza na kuingiza bidhaa kutoka China kwa
kupunguziwa sehemu ya kodi.
“Tumeamua
kuondoa kodi elekezi kwa sababu haina faida kwa taifa na inawanyima
wafanyabiashara wengine, ambao hawaagizi bidhaa kutoka China, fursa ya
kushindana sokoni.
“Serikali
yetu si ya kibaguzi na ndio sababu tumeamua kufuta kodi hii ili kuleta usawa
kwa wafanyabiashara wote,” alisema Kidata.
Aliongeza: “Suala lililopo kwa sasa ni kwa kila mwananchi anayepaswa kulipa kodi katika kitu anachokifanya, alipe kodi na hatutafumbia macho ukwepaji wa kodi na hakuna kitu kinachoitwa kodi elekezi wala msamaha wa kodi katika serikali hii, tulipe kodi kwa maendeleo ya taifa letu.”
Alisema
hakuna sheria yoyote inayosema kuwa kutakuwa na kodi elekezi ama msamaha wa
kodi kwa mfanyabiashara, bali ule ulikuwa ni utaratibu uliowekwa na TRA na
haukuwa na tija.
Katika
hatua nyingine, Kidata alisema serikali ipo kwenye mpango wa kuunda Mamlaka ya
Mapato Kuu ya Taifa nje ya TRA, iliyopo kwa sasa ili kuondokana na malalamiko
ya kero za kodi kwa wananchi wenye kipato cha chini.
Alisema
hiyo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuwasaidia wananchi wa kipato cha
chini, kumudu kulipa viwango vya kodi vinavyowekwa na mamlaka hiyo.
“Serikali
inawajali watu wake na ndio sababu tumeona kuna haja ya kuunda mamlaka moja ya
utozaji wa kodi, itakayojumuisha taasisi zote zinazohusika na ukusanyaji wa mapato
nje ya kodi na ushuru ili kuondoa malalamiko ya wananchi,” alisema.
Kidata
alisema mamlaka hiyo itasaidia kuweka viwango vya kodi, ambavyo wananchi wa
hali ya chini watamudu kulipa kutokana na biashara au kazi wanazozifanya.
TRA
imekuwa na rekodi nzuri ya ukusanyaji wa kodi ila kumekuwa na malalamiko mengi
kutoka kwa wananchi kuhusu kodi, ambazo zimekuwa kero na hazina tija.
Kaimu
Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Salum Yusuf, alisema watalisimamia suala la
ulipaji kodi na yeyote atakayekaidi kulipa, atachukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment