Saturday, 12 March 2016

VIGOGO TISA WASIMAMISHWA KAZI DAWASCO


SERIKALI imeendelea kukunjua makucha yake baada ya kuwasimamisha kazi watendaji tisa wa Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASCO), wakihusishwa na upotevu wa zaidi ya sh. bilioni mbili.

Pia, imeagiza kuchunguzwa kwa Mtendaji Mkuu mstaafu wa mamlaka hiyo, Jackson Midala, kuhusu kashfa hiyo.

Watendaji hao walisimamishwa kazi jana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, alipotembela ofisi za DAWASCO, kwa ajili ya kujitambulisha na kufahamiana na wafanyakazi.

Aidha, aliagiza uchunguzi mzito ufanyike dhidi ya Kampuni ya Ujenzi ya  Strabarg, iliyohusika na ujenzi wa barabara, vituo na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka  (DART), ambayo  inadaiwa kukwepa ulipaji wa bili ya maji, hivyo kuisababishia DAWASCO na serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Waziri Lwenge aliitaka Strabarg kulipa fedha hizo ndani ya wiki mbili na iwapo haitafanya hivyo, itachukuliwa hatua kali za kisheria.

Waziri huyo pia ameiagiza Bodi ya DAWASCO kuvichunguza  viwanda vyote vikubwa vilivyomo Dar es Salaam, kikiwemo Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL) , iwapo vinalipia ankara za maji inavyotakiwa na pia iwapo vina akaunti ya mamlaka na kuitaka bodi hiyo kuwasilisha  ripoti ndani ya wiki mbili.

Aliwataja watendaji waliosimamishwa kazi kuwa ni Meneja Rasilimali Watu,  Mvamo Mandawa, Mameneja Legnard Kessy, Theresia  Mlengu, Emmanuel  Buluba, Rainery Kapera, Peter Chacha, Fred  Mapunda, Bernard  Mkenda na  Jumanne  Ngelela.

Mhandisi Lwenge alisema watendaji hao kwa pamoja wanadaiwa kuhusika katika hujuma ya upotevu wa fedha hizo katika Kampuni ya Strabarg, ambayo ilitumia kiasi kikubwa cha maji wakati wa kutekeleza mradi wa DART.

“Kampuni ya Strabarg ilipewa zabuni ya ujenzi wa mioundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka, uchunguzi umeonyesha kuwa ilitakiwa ilipe sh. bilioni 2.9 za matumizi ya maji ya DAWASCO katika mradi huo, lakini haijalipa,”alisema.

Alisema wapo watendaji pamoja na Mtendaji Mkuu mstaafu Midala, ambao walihusika katika kuyeyuka kwa fedha hizo.

“Huyu Mtendaji Mkuu (Midala) hata kama amestaafu, afuatwe huko aliko na kuhojiwa, ilikuwaje jambo hilo lifanyike. Tunahisi pia fedha hiyo iliyopotea inaweza kuwa zaidi ya sh. bilioni 2.9.

“Watendaji hawa waliosimamishwa leo (jana),waanze kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo. Wanasimamishwa kazi kuanzia leo (jana) ili kupisha uchunguzi na nitataka kupata ripoti ya uchunguzi ndani ya wiki mbili,” alisema huku akionekana kukerwa na suala hilo.

Waziri Lwenge alisema historia ya DAWASCO inaonyesha kuwa, baadhi ya watendaji wake wanahusika katika kuhujumu mapato ya mamlaka, kwa kuchukua fedha katika miradi mbalimbali inayohudumiwa na mamlaka hiyo bila kuziwasilisha kunakohusika.

“Wanaweka maslahi yao mbele kuliko ya mamlaka. Haya ni majipu na tutayatumbua. Uchunguzi umebaini kuna viwanda vingi vikubwa vinatumia maji mengi ya DAWASCO, lakini havina akaunti ya DAWASCO. Wapo wajenzi wa barabara  pia wanatumia maji mengi bila kulipa.

"Tunazo taarifa kuna watendaji  wa DAWASCO  wanachukua fedha hizo katika viwanda na miradi hiyo. Tutawabaini na kuwachukulia hatua kali, ikiwemo kuwahusisha na kesi za kuhujumu uchumi,”alionya.

Aliiagiza Bodi ya DAWASCO kuvichunguza viwanda, ambavyo vinadai vinatumia maji ya visima vikubwa, kama visima hivyo vilichimbwa kwa vibali  na sheria  za mamlaka hiyo.

“Chunguzeni na mnipe majibu ndani ya wiki mbili. Kama kweli kuna visima katika viwanda hivyo, nani aliyewapa leseni ya kuchimba? Kama vimechimbwa kinyume cha sheria, hatua zichukuliwe na kama kuna wahusika kutoka DAWASCO walitoa vibali  kinyume cha taratibu, wachukuliwe hatua," alisema.

Uchunguzi mwingine ambao alitaka ufanyike ni kuhusu Mradi wa Bergiam Tanzania, ambapo baadhi ya watendaji wake wanadaiwa kuuendesha kinyume cha makubaliano.

Akizungumzia ufanisi wa DAWASCO, Mhandisi Lwenge alisema licha ya kuanza kuonekana kwa ufanisi, bado jitihada zaidi zinafanyika ili kuhakikisha  kunakuwepo na ufanisi mkubwa katika kuwapatiwa huduma ya maji wananchi.

“Mradi wa mabomba makubwa wa Ruvu Juu na Ruvu Chini karibia utaanza kufanyakazi na wakazi wa jiji la Dar es Salaam, wataanza kupata maji ya kutosha. Si kwa Dar es Salaam tu, lengo letu ni kuhakikisha kuwa malengo yetu ya wananchi kupata maji ndani ya mita 400 yanafanikiwa,”alisema.

Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka hiyo,  Samweli Kitundu, alimhakikishia waziri  kwamba, watatekeleza maagizo hayo haraka na kwa umakini mkubwa.

Hata hivyo, alimuomba Waziri Lwenge kuisadia DAWASCO katika kutia msukumo kwenye taasisi za serikali zinazodaiwa.

Awali, Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ndani ya mamlaka hiyo,  ikiwemo upotevu  na wizi wa maji, lakini kumekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi kifupi.

“Tuna hakika tunaweza kutekeleza agizo la serikali kwamba ifikapo Mei, mwaka huu, tuwe tumewaunganishia maji wananchi milioni nne,” alisema.

No comments:

Post a Comment