Saturday, 12 March 2016

WATUMISHI WASIOFIKIA MALENGO KUTIMULIWA


SERIKALI imewataka wakuu wa idara zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kuingia mikataba ya kimaandishi na watumishi wote kwa lengo la kuimarisha utendaji.

Chini ya makubaliano hayo, watumishi hao wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na kufikia malengo yanayopangwa na kwamba, endapo mtumishi yeyote atakiuka au kushindwa kufikia malengo yake, atatimuliwa.

Aidha, imeipa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), jukumu la kuhakikisha inakusanya sh.trilioni moja kwa mwaka, badala ya sh. bilioni 652 za sasa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawsiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema hayo jana, Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo.

Aliwataka wakuu wa idara kuhakikisha wanaingia mikataba ya kikazi na taasisi za umma zilizo chini yao ili kuwekeana malengo ya uwajibikaji.

Profesa Mbarawa alisema kama ikitokea mkuu wa kitengo kwenye taasisi, ambazo zitaingia mkataba huo hajatimiza makubaliano hayo, atatimuliwa bila ya kuonewa haya.

“Kumekuwepo na baadhi ya watumishi ambao wanaingia ofisini na kutumia mali za serikali bila kuwajibika, badala yake wanafanya ofisi hizo kama vijiwe.

“Nawaagiza wakuu wa idara kwa mara nyingine kuingia mikataba ya kimaandishi na watumishi wao pamoja na taasisi zilizo chini yao ili ziwajibike ipasavyo. Kama kuna ambaye atashindwa kufikia makubaliano, aachie ngazi kwa kuwa kuna Watanzania wengi hawana ajira,” alisema Profesa Mbarawa.

Aliwataka watumishi wa umma kutambua kuwa wapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na si vinginevyo.

Pia, aliwataka wataalamu wa mifumo ya kielekitroniki kuangalia njia, ambayo wanaweza kuweka mifumo bora itakayomfanyia tathmini kila mtumishi na kumuonyesha akiwa eneo lake la kazi.

Waziri alisema ataongea na taasisi ambazo hazina mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuhakikisha inafungwa na kuanza kutumika ili kumtambua kila mmoja na jinsi anavyowajibika.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza matumizi ya simu za mkononi wawapo kazini, jambo linalochangia kuzorotesha utendaji kazi na ufanisi.

Profesa Mbarawa alisema alitembelea wizarani hapo na kubaini kuwa asilimia 27, ya watumishi wanatumia Youtube, asilimia 37 wanatumia mitandao mingine ya kijamii na asilimia saba tu ndio wanatumia tovuti za kazi wawapo ofisini.

“Kama kweli  watumishi wa umma tumekubali kuwahudumia wananchi, ni lazima tuwe waadilifu kwenye kazi zetu, badala ya kutumia vyombo vya umma kwa maslahi binafsi, tutavitumia kwa ajili ya Watanzania wote.

“Tupo hapa kwa ajili ya kuwajengea Watanzania miundombinu ya kisasa na wanapaswa kutambua kuwa milango ipo wazi kwao muda wote kuleta maoni yao juu ya utendaji kazi wetu,” alisema.

Alitoa wito kwa watumishi wa wizara hiyo kuwa na uhusiano mzuri na taasisi zao ili kufanya kazi zenye tija kwa wananchi.

Waziri huyo alisema kila mmoja atawajibika kulingana na kiwango cha elimu yake na kwamba, haitatokea yeye kuandika ujumbe mfupi kutaka mtu apewe mamlaka ambayo hastahili bali kila mtu anapaswa kufuata taratibu za kazi.

Hata hivyo, aliwaomba wakuu wa idara na wafanyakazi wote kuunga mkono juhudi za serikali za kutaka kukuza uchumi wa nchi kwa kuwajibika ipasavyo na kuleta maendeleo ya kweli chini ya kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.

Aidha, alisema matapeli ambao wamekuwa wakitumia namba za viongozi kutapeli, wameshagundulika na watakamatwa ambapo baadhi yao wameshakamatwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Alisema katika wizara yake, kuna taasisi 29, ambapo ameweza kuongea na taasisi 27 na kati ya hizo, ameongea na mtumishi mmoja mmoja wapatao 70.

Akizungumzia kuhusu TPA, alisema kuanzia sasa haitakubalika kukusanya sh.bilioni 652, kwa mwaka, badala yake wanatakiwa kukusanya angalau sh.trilioni moja, kutokana na marekebisho yaliyofanyika yanayowapa fursa za kukusanya mapato mengi zaidi.

No comments:

Post a Comment