Saturday, 12 March 2016

KIAMA CHA WADAIWA SUGU NYUMBA ZA SERIKALI CHAJA

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ,  Arch. Elius Mwakalinga (kushoto), akikabidhiana hati ya mkataba na Mwakilishi wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart & Co. Ltd, Scollastica Kevela Dar es Salaam leo asubuhi, baada ya kampuni hiyo kushinda zabuni ya kukusanya madeni ya TBA kuanzia leo.

 WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA), wametia saini mkataba wa makubaliano na Kampuni ya Yono Auction Mart, ili kuwaondoa wapangaji walioshindwa kulipa kodi na wale walioshindwa kulipa madeni ya nyumba walizokuwa wameuziwa kwa mkopo.

Hatua hiyo imekuja siku mbili baada ya Waziri wa  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuwapa mwezi mmoja wadaiwa waliokopa nyumba za serikali.

Mkataba huo ulitiwa saini jana, Dar es Salaam, kwa lengo la kukabiliana na watumishi wa umma, watu binafsi na taasisi za umma, ambao wamekaidi kulipa kodi na wengine kushindwa kumalizia mikopo ya nyumba walizonunua.

Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, alisema jana ilikuwa siku ya mwisho kwa wadaiwa hao kulipa fedha hizo
kwamba, hivi sasa jukumu la kuzidai wamelikabidhi kwa Yono.

Alisema kuanzia Machi 16, mwaka huu, Kampuni ya Yono itaanza kuwakamata na kuwatoza faini ya asilimia tano ya nyongeza ya kile, ambacho wadaiwa wote wanatakiwa kulipa.

“Katika mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma, serikali inadai sh.bilioni sita, fedha ambazo zinatokana na madeni ya upangishaji.

"Zingine ni madeni ya  huduma za ushauri, ambazo ni shilingi bilioni 6.9 na madeni ya waliokopa nyumba na hawajamalizia mikopo yao ni shilingi milioni 800," alisema Mwakalinga.

Alitoa wito kwa walioshindwa kulipa fedha hizo, kukopa benki kwa kuwa tayari wameshazungumza na uongozi wa baadhi ya benki, ambazo zimeonyesha utayari wa kuwakopesha wadaiwa hao na kukubali kupunguza riba kutoka asilimia 21 hadi hadi asilimia 15 ili kurahisisha ulipaji.

Alizitaja benki hizo kuwa ni CRDB, BOA NA NMB na kusisitiza kuwa, mdaiwa ambaye hakopesheki benki ni bora aachie nyumba hizo ili kutoa fursa kwa wengine wanaoweza kuzilipia.

Aliongeza kuwa Machi 14, mwaka huu, wanatarajia kumkabidhi Profesa Mbarawa, majina ya taasisi za serikali zinazodaiwa malipo yanayohusiana na masuala ya huduma za ushauri ili aweze kuchukua hatua zaidi kuhakikisha fedha hizo zinalipwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi TBA, Mariam Kazoba, alisema mchakato wa kumtafuta mzabuni atakayehusika na ukusanyaji madeni, ulifuata hatua zote za kisheria, ambapo ulianza Novemba 25, mwaka jana, hadi Februari 23, mwaka huu, ambapo kampuni ya Yono iliibuka mshindi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Yono Auction Mart, Scholastika Kevela, aliwasisitiza wadaiwa wote kulipa madeni yao kabla ya Jumatano ya wiki ijayo, kwani baada ya hapo watasimamia sheria ili kutimiza jukumu lao.

No comments:

Post a Comment