SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
imeahidi kuimarisha maslahi ya wafanyakazi, lakini imeonya kuwachukulia hatua
wale wote ambao ni wazembe.
Ahadi hiyo ilitolewa jana, mjini Zanzibar na
Rais Dk. Ali Mohamed Shein, katika
hotuba yake wakati wa kuzindua rasmi Baraza la Wawakilishi.
Dk. Shein alisema SMZ itaendelea kuimarisha
miundo ya utumishi ili wafanyakazi waendelee kufaidika na elimu, uwezo na
uzoefu walioupata wakiwa kazini na viwango vya elimu walivyonavyo.
Hata hivyo, alisema wafanyakazi wote wanafahamu
kuwa mshahara ni matunda na tunzo mtu anayopata kutokana na juhudi aliyoifanya
katika uzalishaji.
“Kuna baadhi ya watu wamejenga tabia ya kudai
mishahara mikubwa na kuilaumu serikali kuwa haipandishi mishahara bila ya wao
kuwa na ari na dhamira ya kweli ya kujitahidi kufanya kazi na kuzalisha,”
alisema Dk. Shein.
Alisema watu wa aina hiyo wanapaswa kuacha
tabia hiyo, ambayo haina manufaa kwa maendeleo.
Badala yake, Dk. Shein alisema kwa pamoja wanapaswa
kulitekeleza kwa vitendo agizo alilolitoa mwaka 2011, mara tu baada ya kuingia
madarakani kuwa ‘tubadilike na tusifanye kazi kwa mazoea’.
“Tulijitahidi kubadilika na kuyaondoa
mazoea. Lakini ni ukweli usiopingika
matatizo bado yapo, viwango vya utendaji na nidhamu kazini bado havijaongezeka
sana. Ni jukumu letu tufanye kazi kwa bidii na tuipende kazi,” alisema.
Aliongeza: “Wapo baadhi ya wafanyakazi, ambao
hawapendi kufanyakazi (kwa vitendo vyao), na wengine hawataki kufanyakazi,
lakini wao ndio wa mwanzo wanaotaka mishahara mikubwa, posho nzuri, safari za
kila wakati na kuhudhuria kwenye semina na mikutano kila mara.”
Pia, alisena wapo baadhi ya wafanyakazi kwenye
taasisi muhimu zinazotoa huduma kwa wananchi, ambao hawajali kazi zao na
wanakwepa wajibu wao.
“Upo ushahidi kutoka kwa baadhi ya wananchi
kwamba wanapokwenda kutaka huduma wanadharauliwa, wanapuuzwa, wananyanyaswa na
wengine hutakiwa watoe kitu chochote,” alisema.
Dk. Shein alionya: “Wapo baadhi ya watumishi
wenye tabia ya kutoroka, kuchelewa na hawajali kanuni. Wao hujifanya wababe
mbele ya viongozi wao. Wenye sifa mbaya tutawachukulia hatua, kama hapana budi,
tutawafukuza kazini. Hatuwezi kuwa na wafanyakazi waliokuwa na nidhamu.
Sasa basi, imetosha.”
Aliongeza kuwa waliopewa dhamana ya kuongoza idara
mbalimbali za serikali, watapaswa watekeleze wajibu kwa kuwasimamia wafanyakazi
walio chini yao.
Viongozi hao nao wameonywa kuwa kama
hawatawawajibisha wafanyakazi wao, watawajibishwa wao.
Pia, Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa atatekeleza
ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015, za kuimarisha
maslahi ya wafanyakazi katika sekta mbalimbali, ukiwemo utoaji wa kima cha
chini cha mshahara cha sh. 300,000 kwa mwezi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja
baada ya kuingia madarakani.
Alisema katika kipindi cha uongozi wake, serikali
itaimarisha huduma za hifadhi ya jamii kwa wanachama wake, kwa kubuni utoaji wa
mafao mapya na kuongeza kiwango cha malipo ya kiinua mgongo na pensheni.
“Madeni ya viinua mgongo vya wafanyakazi
waliostaafu tutayalipa, tunawaomba wastaafu wawe na subira,” alisema Dk. Shein.
Kuhusu ajira, alisema suala hilo bado ni
changamoto kama ilivyo katika mataifa mengine na kwamba, ana matumaini makubwa
ya kupata mafanikio katika ongezeko la nafasi za kazi katika kipindi kijacho
kutokana na mikakati iliyopo.
“Tutahakikisha jitihada za serikali za
kutekeleza mageuzi ya uchumi zinafanikiwa katika sekta ya utalii na viwanda kwa
kuwashajiisha wawekezaji,” aliahidi na kuongeza kuwa, sekta binafsi itaimarishwa
na kuwa chanzo kikuu cha ajira.
No comments:
Post a Comment