Wednesday 6 April 2016

RAIS MAGUFULI ZIARANI RWANDA



Rais Dk. John Magufuli, leo anaanza ziara yake ya kwanza ya kikazi nje ya nchi kwa kutembelea Rwanda.

Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ilisema  Rais Dk. Magufuli atakuwa na ziara ya siku mbili, yaani leo na kesho nchini Rwanda kwa mwaliko wa Rais Paul Kagame.

Katika ziara hiyo, taarifa ilisema viongozi hao watashiriki katika uzinduzi wa Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha Mpakani, chenye huduma zote muhimu kwa pamoja kama ilivyokubaliwa na nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).

Huduma za kituo hicho cha mpakani zinatajwa kuwa ni muhimu katika kuharakisha shughuli kati ya nchi hizo mbili, lakini pia kuziunganisha nchi za Mashariki na Afrika ya Kati, ambazo hazina bandari.

Taarifa ilisema baada ya hafla hiyo, viongozi hao watakwenda mjini Kigali, ambako watafanya mazungumzo na baadaye kuweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Hii itakuwa safari ya kwanza nje ya nchi kwa Rais Dk. Magufuli, tangu alipochaguliwa kuwa rais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka jana.

No comments:

Post a Comment