ENEO la Feri jana lilighubikwa na simanzi kufuatia taarifa za watu wawili kufariki dunia, baada ya gari walilokuwa wakivuka nalo kwenye kivuko cha MV. Kigamboni, kuserereka na kuzama baharini.
Tukio hilo lilivuta umati mkubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali, ambao walikuwa wakifuatilia shughuli za uokoaji na uopoaji wa miili ya watu hao, uliokuwa ukifanywa na vikosi vya Jeshi la Zimamoto, Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamishna Mwandamizi wa Jeshi la Polisi na Kikosi cha Wanamaji, Mboje Kanga, alisema tukio hilo lilitokea jana, saa 9.30, alfajiri.
Kanga alisema ndani ya gari hilo aina ya Toyota Hiace, alikuwemo dereva, ambaye ametambulika kwa majina ya Dani Stephano (35), mkazi wa Temeke, akiwa na abiria aliyetambulika kuwa ni Nice Kalago (53),mkazi wa Tukuyu, Mbeya, ambao walizama muda mfupi baada ya kuingia kwenye kivuko.
Alisema miili ya marehemu hao imepatikana kwa nyakati tofauti na kwamba, mwili wa mwanaume ulikuwa wa kwanza kupatikana saa tatu asubuhi na wa mwanamke huyo ulipatikana saa nane mchana, huku gari likiwa limeonekana lilipo, hivyo meli ya mizigo ilikuwa ikisubiriwa ili kuliopoa.
Kaka wa marehemu Nice, Brown Mwakalago alidai walikuwa wanatoka kwenye msiba wa kaka yao Mbeya, ambapo walirudi Dar es Salaam, kwa lengo la kuhamishia msiba nyumbani kwa marehemu Kigamboni, alipokuwa akiishi enzi za uhai wake.
Alisema Nice, ambaye ni mdogo wake na ndugu wengine, iliwalazimu kupanda magari ya mchana yaliyokuwa yakitoka Mbeya kwenda Dar es Salaam, ambapo walifika usiku.
Mwalago alisema baada ya kufika, walikuta kivuko kimefika, ambapo waliomba kwenda kuweka mizigo waliyokuwa nayo maana kilikuwa hakijaruhusu watu kuingia wala magari.
“Tuliomba walinzi wa pale kupeleka mizigo yetu kwa kuwa ilikuwa mikubwa, ambapo walitukubalia na tulipomaliza kuipeleka kwenye kivuko, tulirudi eneo la kusubiri turuhusiwe kuingia, ndipo dada, ambaye ni marehemu akawa analalamika anajisikia vibaya na hawezi kusimama.
"Kuna Hiace ilikuwa inasubiri kuingia kwenye kivuko, ndipo tulipoomba msaada, ambapo dereva alikubali na kumpandisha ndani ya gari hilo,”alisema.
Alidai baada ya muda kivuko kiliruhusu watu na magari yaingie, ambapo waliingia, lakini kutokana na watu kuwa wachache, ilibidi kisubiri kijae. Alisema baada ya robo saa toka waingine ndani ya kivuko hicho, walishangaa kuona ile hiace iliyokuwa imesimama ndani ya kivuko hicho ikisesereka na kuzama baharini.
Kwa upande wake, Sajenti Abdul Swani kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, alisema walipoingia mara ya kwanza, walifanikiwa kupata mwili mmoja wa mwanaume, lakini kutokana na mawimbi yaliyokuwepo, ilikuwa ikisogezwa mbali.
“Baada ya kuona hamna dalili ya kuupata mwili wa pili, tulikwenda umbali zaidi wa mita 13, maana mwanzo tuliupata mwili wa kwanza urefu wa mita 8 hadi 9, lakini hatukuuona mwili wala gari. Tunashukuru majira ya saa nane, tulifanikiwa kupata mwili wa pili, ambao tuliukuta ndani ya gari hilo, ndipo tulipoutoa na kuacha gari ili meli za kuchukua mizigo zije kulitoa,”alisema.
Mashuhuda wengine walinukuliwa na gazeti hili wakidai kuwa, kuzama kwa gari hilo kumetokana na uzembe wa watumishi wa vivuko kutokufunga kizingiti kama inavyotakiwa na kuiomba serikali kuchukua hatua dhidi yao maana imekuwa si mara ya kwanza kuzama kwa gari au watu, hali inayosababishwa na uzembe.
No comments:
Post a Comment