MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,
ameahidi kutoa donge nono la sh. milioni 15, kwa mwalimu
wa somo la sayansi katika shule za sekondari, ambaye mwanafunzi wake atafanya
vizuri mtihani wa kidato cha pili.
Aidha, Makonda ameahidi kutoa zawadi ya kitita cha sh.
milioni 10, kwa mwalimu, ambaye wanafunzi wake watafanya vizuri kitaifa katika
somo la sayansi.
Pia, amesema atatoa zawadi ya sh. milioni tano kwa
mwalimu wa sekondari, ambaye wanafunzi wake watafaulu vizuri somo lake kitaifa.
Makonda, alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki, Dar es
Salaam, katika hafla ya uzinduzi wa udhamini kwa wanafunzi kutoka kaya
masikini, wanaosoma katika shule za serikali, unaoendeshwa na shule za Feza.
Mkuu huyo wa mkoa ametangaza ofa hiyo siku chache baada
ya kuwaanzishia walimu wote wa shule za serikali katika mkoa wa Dar es Salaam,
utaratibu wa kupanda mabasi ya daladala bure.
Makonda alisema ameamua kutangaza ofa hiyo kwa walimu wa
mkoa huo kutokana na kutambua umuhimu na uzito wa kazi yao.
“Pamoja na kutoa motisha
hiyo, mwalimu atakayefaulisha wanafunzi wake vizuri kitaifa, nitampa ofa ya
kwenda kutalii katika mbuga yoyote ya wanyama, yeye na familia yake ya watu
watatu,”alisema.
Makonda alisema kwake hakuna tatizo la fedha kwa sababu
wadau mbalimbali wa elimu nchini, wameamua kuisaidia serikali yao, hivyo
chochote anachokihitaji, hujitokeza kumsaidia.
“Watu hivi sasa
wanaichangia serikali yao, tofauti na awali. Ndiyo maana ninasema pesa siyo
tatizo.
“Awali walikuwa wanatoa fedha, lakini zililikuwa
hazitumiki ipasavyo. Zilikuwa zinaishia katika mifuko ya wajanja wachache,” alibainisha.
Aliupongeza uongozi wa shule za kimataifa za Feza, kwa
kubuni programu muhimu ya kuwasaidia wanafunzi wanaotoka katika kaya
masikini na kuwataka wanafunzi waliopata
fursa hiyo kutobweteka.
“Wanafunzi msome kwa bidii ili msiwavunje moyo wadhamini hawa. Pia nitoe wito kwa wazazi
kuendelea kuchangia elimu, hata kama huna uwezo wa kuchangia, basi fanya hata
maombi kwa Rais Dk. Magufuli, ambaye anafanyakazi kubwa kuhakikisha nchi yetu
inasonga mbele,”alisema Makonda.
Mkurugenzi Mkuu wa shule za Feza, Issa Otcu,
alisema, programu hiyo ya
kusaidia wanafunzi wa shule za msingi wanaotoka katika kaya masikini, itagharimu
sh. milioni 37.5, kwa mwaka huu.
Alisema program hiyo inajumuisha wanafunzi 150, kutoka
shule mbalimbali za msingi mkoani Dar es Salaam, ambapo kila mwanafunzi
ataingiziwa sh. 250,000, katika akaunti
yake, zitakazomsaidia kupata mahitaji
muhimu ya shule, ikiwa ni pamoja na kununua sare.
“Nia yetu ni kuunga mkono jitihada za Rais wetu Dk. John
Magufuli katika kutekeleza sera yake ya
elimu bure. Kama wadau, tumeona tuna wajibu mkubwa wa kushiriki katika
kufanikisha hilo, ambapo mpaka sasa
tumewaingizia wanafunzi hawa shilingi milioni moja katika akaunti
zao,”alisema Otcu.
No comments:
Post a Comment