VIONGOZI na
wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), wametakiwa kuzitambua na
kuzisimamia rasilimali za umoja huo ili
zitumike kwa manufaa ya umoja huo na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo
yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UWT, Said El- Maamry,
alipozungumza na wajumbe wa Baraza la Utekelezaji la umoja huo wa wilaya ya
Kinondoni, Dar es Salaam.
El-Maamry alikuwa
katika siku ya mwisho ya ziara ya siku tatu ya kukagua mali za UWT mkoani Dar
es Salaam, akiwa amefuatana na Katibu Mkuu wa umoja huo, Amina Makilagi na mjumbe
wa Baraza Utekelezaji, Angella Kairuki.
Alisema UWT
inazo rasilimali za kutosha, vikiwemo viwanja na majengo, lakini haziunufaishi
umoja huo na CCM, kutokana na usimamizi
dhaifu wa viongozi wake.
Aidha,
alisema kutotumika kwa rasilimali hizo kuunufaisha umoja huo na Chama, pia kumechangiwa
na viongozi wake kutokuwa wabunifu wa kuifanya miradi hiyo kuwa endelevu na
yenye tija.
Alisema
kutokana na udhaifu wa baadhi ya viongozi na watendaji, majengo na viwanja vya
umoja huo, havina hati na kusababisha katika baadhi ya maeneo rasilimali hizo
kuvamiwa na kusababisha mgogoro kati ya wananchi na UWT.
El-Maamry
alisema hata miradi ya ubia kati ya UWT na wawekezaji, iliyoko katika baadhi ya
matawi, kata, wilaya na mikoa, haiunufaishi umoja huo kutokana na baadhi ya
viongozi na watendaji kutokuwa waadilifu.
Aliwataka
viongozi na watendaji wa UWT katika ngazi zote, kuwa wabunifu wa kuanzisha
miradi katika viwanja na majengo kwa kushirikiana na wawekezaji, wakizingatia
kuweka mbele maslahi ya UWT na CCM wakati wa kutia saini mikataba na wawekezaji
hao.
Kwa upande
wake, Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi, alisema uamuzi wa kukagua mali za UWT
ni agizo la CCM ili kutambua changamoto zilizopo, ili ifikapo mwaka 2019, umoja
huo ujitegemee katika uendeshaji, ikiwemo mishahara ya watumishi wake.
Amina
alisema ziara hiyo ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini kukagua mali za UWT,
imeanzia mkoa wa Dar es Salaam, kwa kutembelea wilaya za Temeke, Ilala na
Kinondoni, na itaendelea katika mikoa yote nchini.
No comments:
Post a Comment