Na
Mwandishi Maalum
MAKAMU
wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali haina nia ya kumwonea mtu
inapochukua hatua ya kutumbua majipu kwa watumishi wa umma.
Samia,
alisema hayo juzi, baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Morogoro, iliyosomwa na
Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Steven Kebwe, akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku
tatu mkoani humo.
Alisema
lengo la kutumbua majipu ni kurekebisha na kurejesha nidhamu, uadilifu na uwajibajikaji
serikalini kama ilivyoangizwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili
Watanzania wote wafaidike na matunda ya nchi yao.
"Mtasikia
katika serikali tunarekebisha, majipu yanatumbuliwa, kwa kweli hatuna nia ya
kumwonea mtu, tunarekebisha kama ilivyoagizwa katika Ilani yetu ya Chama Cha
Mapinduzi ili Watanzania wote wafaidi matunda ya nchi yao," alisema.
Makamu
wa Rais alisema katika marekebisho hayo, serikali imechukua hatua ya kukata
mishahara ya walio juu na kunyanyua ya walio chini ili waje juu kidogo na
kwamba, jitihada zote hizo ni katika kufanya mambo yaende vizuri nchini.
"Tunapozungumzia
amani na utulivu ni pamoja na kuhakikisha kwamba walio chini wapo vizuri. Wasipokuwa
vizuri hakuna amani na utulivu, kazi itawapata watu wa kamati ya ulinzi na
usalama kuwatuliza kila siku na hawatatulizika kwa sababu wana shida,"
alisema Makamu wa Rais na kuongeza:
"Lakini
tukiwatuliza kwenye mambo yao wana maji, wana umeme, wana chakula, mtoto
anaenda shule vizuri, anapata afya, akienda zahanati dawa zipo, watatulia
tu."
Alisema
kwa sasa kuna tatizo la watumishi hewa na wengine wamediriki kumdanganya mkuu
wao wa kazi na hayo ndiyo mambo ambayo hayaleti picha nzuri katika serikali.
Aliwataka
wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuunga mkono jitihada hizo za serikali ili
kurejesha nidhamu na uwajibaikaji kwa watumishi wote.
Wakati
huo huo, Makamu wa Rais jana alitembelea kiwanda cha kutengeneza nguo cha
Mazava, ambapo aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuzingatia masharti ya ajira
na wafanyakazi kuchapa kazi kwa bidii ili Taifa liweze kupata kodi na wao
wapate mapato.
Akizungumza
na wafanyakazi, Samia aliuhakikishia uongozi wa kiwanda hicho kuwa, serikali
itazifanyia kazi changamoto za eneo na ukosefu wa ujuzi kwa kuwapeleka vijana
wengi kwenye Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) kujifunza ushonaji.
Alisema
serikali ya awamu ya tano imeweka mkazo kwenye viwanda na kusisitiza kwamba,
kupitia mpango wa EPZ, viwanda vingine vinatarajiwa kujengwa mkoani humo, jambo
ambalo litaongeza ajira kwa vijana.
Kiwanda
hicho ambacho kilianza uzalishaji mwaka 2010, kina wafanyakazi zaidi ya 2,000
na kwamba, asilimia 100 ya nguo zinazozalishwa kiwandani hapo zinauzwa nje ya
nchi, ambapo soko kuu liko Marekani.
No comments:
Post a Comment