CHAMA cha CUF kimeingia
kwenye mpasuko kutokana na kuibuka kwa makundi yanayokinzana ndani ya chama
hicho.
Imeelezwa kuwa kutokana na kuzuka
kwa makundi hayo, wanachama wamedhamiria kurejeshwa kwenye uongozi, aliyekuwa
Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Habari za kuaminika kutoka
ndani ya chama hicho zimeeleza kuwa, ili kufanikisha mpango huo, wanachama, wapenzi na mashabiki wametakiwa
kuanzisha vuguvugu hadi Profesa Lipumba arudishwe kukiongaza chama hicho.
Wakizungumza katika
kongamano la CUF, lililofanyika jana,
Manzese, Dar es Salaam, baadhi ya viongozi na wanachama walisema wanamhitaji
Profesa Lipumba arudi ndani ya chama hicho.
Rashid Athumani, mwanachama
kutoka Mtwara, aliwataka wanachama, wapenzi na mashabiki kuanzisha vuguvugu
hadi Profesa Lipumba arudi kwenye chama hicho.
Alisema wanachama wanamhitaji
kiongozi huyo na kwamba, aliamua kukaa pembeni baada ya kuona mapungufu kwenye
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Aliongeza kuwa ndani ya
UKAWA, kulikuwa na mapungufu, hivyo Profesa Lipumba aliamua kujiweka pembeni.
Mjumbe wa Baraza Kuu la
CUF, Masoud Mhina, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mabanda mkoani Tanga,
alisema wakati umefika kwa chama hicho kuwa na viongozi wenye uwezo wa kuongoza
ndani na nje ya nchi.
Alisema uchaguzi
umemalizika, hivyo ni wakati sasa viongozi na wanachama kukijenga chama kwa
ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
“Uchaguzi umemalizika, tuliingia
kwenye misingi ya UKAWA, ingawa kuna changamoto zake, hivyo ni vyema tukajenga
chama chetu,” alisema.
Ashura Mustapher, ambaye ni
Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, aliwataka wanachama kujiepusha na makundi yenye
lengo la kukigawa chama hicho.
Alisema makundi ndani ya
chama hayaepukiki, lakini yasiyokuwa na tija ni vyema yakaepukwa.
Mkurugenzi wa Ulinzi na
Usalama wa CUF, Mustapher Wandwi, aliwataka wanachama wasikubali kutengana na
kwamba, iwapo watatengana, wanaweza kusababisha mpasuko mkubwa.
“Ninawaomba wanachama
wenzangu tujiepushe kujiingiza kwenye makundi kwani yanaweza kukiingiza chama
kwenye matatizo,” alisema.
Alisema iwapo wanachama
wanataka kufanya mabadiliko ya uongozi, hakuna tatizo, lakini wanapaswa kuchagua
kiongozi ambaye wanamfahamu.
Wandwi aliwataka wanachama
wasikubali kubaguliwa kutokana na suala la uongozi kwani viongozi wa ngazi za
juu wa chama hicho ni kitu kimoja.
“Suala la uongozi msikubali
kuchanganywa kwani Maalimu Seif, Lipumba na Duni (Juma) ni kitu kimoja na siku
zote wako pamoja,” alisisitiza.
Alisema Profesa Lipumba
alijivua uongozi, lakini hajatoka ndani ya CUF na kwamba, hadi sasa anashiriki
vikao vya chama hicho.
Aliwataka wanachama
wasikubali kutengana kwani wakifanya hivyo, watagawanyika na kusababisha
mpasuko.
Mmoja wa wanachama, ambaye
hakufahamika jina lake, alisema ndani ya chama hicho kuna uonevu mkubwa na
kwamba viongozi wanawakandamiza wanachama wa chini.
Alisema katika uchaguzi
uliopita, waliingia kwenye uchaguzi bila kuwa na bendera.
Mwanachama huyo alisema ni
vyema uonevu huo ukaondolewa ndani ya chama hicho ili kukiacha kikiwa salama.
“Ndani ya chama chetu kuna
makundi, ambayo si mazuri na yanakiweka chama kwenye wakati mgumu,” alisema.
No comments:
Post a Comment