Monday, 18 April 2016

MAKONDA ABAINI UFISADI WA KUTISHA DAR




MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameibua ufisadi mkubwa  uliokuwa ukifanywa na  Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam,  Wilson Kabwe na  Kaimu Mkurugenzi wake, Sarah Yohana,  ambapo ameagiza mamlaka husika kuwaondoa haraka.
Makonda amesema vigogo hao wameisababishia  serikali hasara ya sh. milioni 500, katika kipindi cha mwaka mmoja, kutokana na kuingia mikataba mbalimbali mibovu.
Ameitaja mikataba hiyo kuwa ni pamoja na ya zabuni mbalimbali, kinyume cha sheria, zikiwemo kampuni  inayokusanya ushuru katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo na kampuni ya kukusanya ushuru wa maegesho jijini Dar es Salaam (NPS).
Kufuatia kuibua ufisadi huo, Makonda amesema hataki tena kufanya kazi na vigogo hao katika jiji la Dar es Salaam na kuzitaka mamlaka husika kuwachukulia hatua haraka.
Ufisadi stendi ya Ubungo
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, jana, Makonda alisema uchunguzi uliofanyika katika stendi ya Ubungo, umebaini kuwepo udanganyifu mkubwa,  kuanzia katika mikataba ya halmshauri ya jiji na mzabuni aliyechukua jukumu la kukusanya ushuru.
Alisema halmshauri ya jiji na mzabuni huyo wanatumia mikataba miwili tofauti,  ambapo kampuni iliyochukua tenda inatumia mkataba unaoongozwa na sheria ya mwaka 2009, wakati upande wa jiji wanakusanya mapato kwa mzabuni huyo kwa kutumia sheria iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004.
“Sheria ya mwaka 2004, inaitaka kampuni inayochukua zabuni katika stendi hiyo kulilipa jiji sh. milioni 42, kwa mwezi. Sheria hii ilirekebishwa mwaka 2009, ambapo kampuni ilitakiwa kulilipa jiji sh. milioni 84, kwa mwezi,”alisema Makonda.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo  iliyochukua zabuni   stendi ya Ubungo, inatumia mkataba wa mwaka 2009, unaoitaka kulipa sh.milioni 84, lakini inapokwenda kulipa jiji, inatumia mkataba wa  mwaka 2004, hivyo kulipa sh. milioni 42, kinyume na utaratibu.
“Kwa maana hiyo, serikali inapoteza sh. milioni 500, kila mwaka. Fedha hizi nyingi zinaishia mikononi mwa wajanja wachache wakati Watanzania wanakabiliwa na matatizo mengi. Hatuwezi kuvumilia,” alisema.
Makonda alisema udanganyifu mkubwa ulikuwa ukifanywa na Mkurugenzi wa Jiji,  Kabwe na Kaimu wake,  Sarah, ambao walifikia hatua ya kusaini mikataba miwili tofauti katika zabuni moja kwa kampuni moja.
“Kufuatia ufisadi huu mkubwa uliokuwa  ukifanywa na hawa watu, mimi  kama mkuu wa mkoa sitaki tena kufanya nao kazi. Mamlaka husika ziwaondoe haraka. Hatuwezi kufanyakazi na watu ambao wanakwamisha kwa makusudi jitihada za serikali yetu,”alisema Makonda.
Ufisadi NPS
Kuhusu mkataba wa kampuni ya kukusanya ushuru wa maegesho ya magari ya NPS, Makonda alisema katika hali ya kusikitisha, Mkurugenzi huyo wa jiji na kaimu wake, waliiongezea muda kinyume na utaratibu na sheria ya zabuni za serikali.
Alisema kampuni hiyo ilikwishamaliza muda wake mwaka jana, lakini katika hali inayoonyesha vigogo hao wana maslahi na kampuni hiyo,  waliiongezea muda wa miezi sita kwa madai kuwa,  jiji halijapata mzabuni mwingine wa kufanyakazi hiyo.
“Septemba Mosi, mwaka jana,  jiji liliiongezea muda  kampuni hiyo wa miezi sita zaidi wakati ni kinyume cha sheria, inayotaka zabuni kutangazwa mara moja kampuni inapomaliza muda wake,”alibainisha mkuu huyo wa mkoa.
Aidha, alisema baada ya miezi sita kumalizika, vigogo hao waliiongezea tena kampuni hiyo muda wa miezi mitatu wa kuendelea kukusanya ushuru wa maegesho kinyume cha sheria.
“Hawa ni viongozi gani?  Jambo hili si kwamba  linatuptezea mapato, lakini pia linavunja moyo.  Huwezi kuongeza muda wa zabuni wakati sheria ipo. Nataka waondolewe,”alisema Makonda.
Mkuu huyo wa mkoa pia aliinyooshea kidole   kampuni ya NPS, kutokana na kukiuka haki za wafanyakazi wake wanaofanya kazi ya kukusanya ushuru katika maegesho.
Wizi Tambaza
Makonda pia aliigusia kampuni ya udalali ya Tambaza, kwa kuishutumu  kuwaibia waziwazi  wapanda pikipiki, maarufu kama bodaboda, kwa kuwatoza  faini ya sh. 80,000, badala ya  sh.20,000, iliyopangwa kisheria.
“Tumechunguza na kubaini kwamba, Tambaza hawawatendei haki kabisa wananchi wenye pikipiki.  Faini wanayowatoza ni kubwa kuliko inayotozwa na askari wa usalama barabarani. Hili halikubaliki. Tutachukua hatua,”alisema.
Atoa onyo
Mkuu huyo wa mkoa amesema, wakati Rais Dk. John Magufuli na watwendaji wake,  wanahangaika kuhakikisha wananchi wanapata maisha nafuu kwa kubana bajeti na kuelekeza fedha katika miradi ya kijamii, kampuni hizo na baadhi ya watendaji wa jiji, wamekuwa wakichezea fedha za umma, hivyo kuna kila sababu ya kuwawajibisha kikamilifu.
Alisema tayari  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeanza mara moja kuwachunguza wahusika wote wa mikataba iliyoitia hasara serikali pamoja na kuchunguza ubadhirifu huo mkubwa wa fedha.

No comments:

Post a Comment