Monday 11 April 2016

WASOMI WAPONGEZA UTEUZI WA BARAZA LA MAWAZIRI ULIOFANYWA NA DK. SHEIN




BAADHI ya wasomi nchini wamepongeza uteuzi wa Baraza la Mawazili la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kusema kuwa, linaundwa na sura zilizo tayari kuleta maendeleo ya haraka.
Wamesema kulingana na uteuzi huo, Zanzibar inaweza kuingia kwenye nchi chache za Afrika, ambazo zitakuwa na uchumi unaokuwa kwa kasi ya uongozi wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein.
Kwa upande wao, Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamesema baraza hilo limebeba matarajio na kwamba, waamini litawavusha kwenye nyanja mbalimbali.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Dk. Shein kuteua baraza jipya la mawaziri, huku akiwajumuisha kwenye serikali yake baadhi ya wanasiasa wa upinzani.
Wasomi hao walisema sababu kubwa ya kutokea hali hiyo ni umoja na mshikamano utakaojengwa kwa jitihada zote za serikali hiyo, baada ya kupita kwenye kipindi kigumu kilichotokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015.
"Ni lazima watajituma sana kurudi kwenye hali yao ya kawaida. Kile kipindi cha mpasuko wa kisiasa kitakuwa ndio chachu ya mafanikio hayo, naamini hivyo," alisema mmoja wa wasomi hao.
Dk. Phinias Rwegoshora, Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Ruaha, alisema mara nyingi tofauti na matarajio ya watu, nchi zinazopitia kwenye matatizo hurudi na kuwa na nguvu kiuchumi.
Alisema historia inaonyesha kuwa, nchi za Ulaya, ambazo hali yao ya uchumi ilikuwa mbaya zaidi kipindi cha vita kuu za dunia, wananchi wake licha ya mpasuko, walirudi na kushirikiana kuchapakazi.
Aidha, alisema hatua aliyochukua Rais Dk. Shein kuwajumuisha wapinzani kwenye baraza lake la mawaziri, ni ya busara na kwamba kila kiongozi anapaswa kuiiga.
"Kama nilivyosema Wazanzibar wameiamini busara ya Rais wao kwa sababu hali ni tulivu tangu kukamilika kwa uchaguzi wa marudio na sasa serikali imepatikana, tuwaombee," alisema.
Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema uundwaji wa baraza jipya la mawaziri la SMZ, una maana kuwa Dk. Shein amekamilisha jukumu la kikatiba la kuunda chombo kitakachomsaidia kuendesha serikali.
Alisema sura zilizomo kwenye baraza hilo zinaleta matumaini makubwa kwa Wazanzibar na Wabara kuwa, itakuwa serikali yenye jukumu kuu pamoja na mengine, kuboresha mshikamano na umoja wa raia.
Aidha, alisema walioteuliwa kuunda baraza hilo ni watu wazoefu, wanayoijua Zanzibar na Mapinduzi, hususan umuhimu wake kwa Wazanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Pamoja na hayo, Bana alisema kitendo cha Dk. Shein kuwajumuisha wapinzani kwenye baraza lake, akiwemo Hamad Rashid Mohammed, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya ADC, ameonyesha utayari kwenye kushirikiana kuijenga Zanzibar bila ubaguzi.
"Hamad Rashid ni mzoefu kisiasa, kaonyesha ukomavu kwenye bunge maalumu la katiba kwa kutoa hoja makini, hivyo kumpa wizara ni kuchagua njia sahihi kwa wakati sahihi.
"Kingine Hamad Rashid hana utamaduni wa kuendekeza ushindani wa kisiasa kwa kufa na kupona ili tu awe madarakani, ni mtu anayefanya jambo kwa maslahi ya taifa, hivyo atakuwa msaada mkubwa kwa SMZ," alisema.
Alisema katika baraza hilo, mawaziri wawili miongoni mwa wateule ni wapinzani, ambao wamepewa uwaziri usio na wizara maalumu, hivyo fursa zimetolewa bila kuzingatia itikadi, jambo ambalo ni afya kwa serikali.
Alisema Wazanzibar watarajie serikali makini na kwamba, waache mivutano iliyokuwepo wakati wa uchaguzi, washikamane na kusonga mbele kuijenga nchi yao.
Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Diplomasia (CFR), kilichoko Dar es Salaam, walisema SMZ imekamilika, hivyo kilichobaki wateule waunde nguvu ya pamoja kujenga serikali madhubuti itakayokuwa na sura nzuri kimataifa.


Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, akizungumzia kuhusu baraza hilo, alisema lina kila dalili ya kuleta maendeleo na kwamba, limezingatia matakwa mbalimbali ya vijana.
Shaka alisema walioteuliwa kwenye baraza hilo wana taaluma, upeo, uzoefu na uzalendo wa kuitumikia Zanzibar na kuiletea maendeleo.
Alisema Rais Dk. Shein amekonga nyoyo za wananchi, ambao walitaka kuwepo mabadiliko kwenye baraza hilo ili kusukuma mbele maendeleo ya Zanzibar kwa haraka.
"UVCCM tunaliita  ni baraza la mageuzi na  mafanikio endelevu, tungependa kuona kila waziri akionyesha uwezo wake," alisema Shaka.
Alisifu uteuzi huo na kusema kuwa, kama wataamua kufanya kazi bila muhali,  kukataa kazi kwa mtindo wa mazoea au kusubiri hadi waziri aamrishwe na Rais, itakuwa kazi bure, lakini anaamini ni timu mpya ya wachapakazi  iliyosheheni vijana mahiri.
Hata hivyo, alisema UVCCM kwa kuwa ni jumuia ya Chama, haitaacha kukosoa, kushutumu na kupaza sauti pale itakapoona mambo hayaendi sawa, kutokana na kiwingu ama cha walaji, wafujaji na wazembe wanaosaliti sera za serikali na misimamo ya CCM.
DK. SHEIN AWAAPISHA
Wakati huo huo, Rais Dk. Shein, jana aliwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri wa wizara 13, wakiwemo mawaziri wasiokuwa na wizara maalumu, ambao pia ni wajumbe wa Baraza la Mapinduzi.
Hafla hiyo ilifanyika jana, katika viwanja vya Ikulu mjini Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasaa, serikali pamoja na wananchi.
Miongoni mwa waliohudhuria ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid.
Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Said Hassan Said, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Khamis Haji, Mkuu wa  Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis, Meya wa Manispaa ya Mji wa Unguja, Khatib Abrahman Khatib pamoja na viongozi wa vikosi vya ulinzi na usalama.
Walioapishwa katika hafla hiyo ni Waziri, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Gavu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ, Haji Omar Kheri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohammed, Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma.
Pia wamo Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Moudline Castico,Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Balozi Ali Abeid Karume, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohammed.
Wengine ni Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Rashid Ali Juma na Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Salama Aboud Talib.
Kwa upande wa manaibu waziri walioapishwa ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Khamis Juma Maalim, Naibu Waziri wa Afya, Harusi Said Suleiman na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri.
Wengine ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mohammed Ahmed Salum, Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Lulu Msham Abdulla, Naibu Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Choum Kombo Khamis na Naibu Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Juma Makungu Juma.
Aidha, Dk. Shein amewaapisha Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi na Mawaziri Wasiokuwa na Wizara Maalumu, akiwemo Said Soud Said kuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri Asiyekuwa na Wizara Maalumu pamoja na Juma Ali Khatib, Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri Asiyekuwa na Wizara Maalumu.
Kwa uwezo aliopewa chini ya vifungu 42, 43,44 na 47 vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Dk. Shein ameunda wizara 13 za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwateua mawaziri na manaibu mawaziri wa wizara hizo pamoja na mawaziri wasiokuwa na wizara maalumu na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi.

No comments:

Post a Comment