Monday 11 April 2016

WALIOHUSIKA KUWALIPA WATUMISHI HEWA WAADHIBIWE-MAJALIWA



WAZIRI Mkuu  Kassim Majaliwa amewataka makatibu tawala wa mikoa nchini kuchukua hatua kali kwa wote waliosababisha kuwepo kwa watumishi hewa.

Amesema suala hilo la watumishi hewa limeisababishia serikali hasara kubwa, hivyo ni lazima waliohusika katika mchakato huo wabainishwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za utumishi.

Majaliwa aliyasema hayo jana, alipokuwa akipokea taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Lindi, iliyowasilisha na Mkuu wa mkoa huo, Godfrey Zambi, katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi wilayani Ruangwa .

Rais Dk. John Magufuli wakati akiwaapisha wakuu wapya wa mikoa, Machi 15, mwaka huu,  aliwapa siku 15 kuhakikisha wanawabaini watumishi hewa wote katika mikoa yao na kuwaondoa katika mfumo wa malipo.

Baada ya kufanyika kwa zoezi hilo, jumla ya watumishi hewa 7,795, walibainika, ambao wameisababishia serikali hasara ya  sh. bilioni 7.5.

Waziri Mkuu alisema operesheni ya kubaini watumishi hewa inalenga kuokoa fedha za serikali zilizokuwa zikitumika kuwalipa watumishi waliokufa, kustaafu na wale, ambao wahusika walijiwekea majina na kisha fedha kuingia mifukoni mwao.

“Makatibu tawala  wa mikoa ndio wakuu wa watumishi katika mikoa, hivyo ni lazima tusikie wamechukua hatua gani kwa wote waliosababisha kuwepo kwa watumishi hewa na si kukaa wakisubiri maagizo ya rais,” alisema.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, katika taarifa yake kwa Waziri Mkuu, alisema mkoa huo una jumla ya wafanyakazi watoro 57 na hewa saba, ambao ni marehemu na  wastaafu waliokuwa wanalipwa mishahara na kuisababishia serikali hasara ya sh. milioni 36 kwa mwezi mmoja.

Alisema utaratibu wa kubaini watumishi hewa na watoro utakuwa endelevu na kwamba, wameanzisha timu kwa ajili ya kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha watumishi waliokufa au kustaafu kuendelea kulipwa.

No comments:

Post a Comment