Tuesday 31 May 2016

MASAUNI AAGIZO MAOFISA UHAMIAJI KITENGO CHA UPELELEZI WAONDOLEWE


NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Massauni, ameagiza kupewa barua za kuondolewa kazini mara moja watumishi wa Uhamiaji kitengo cha upelelezi, ambao wameshindwa kwenda sambamba na kasi.

Pia, ameagiza kupitiwa upya kwa mikataba yote inayohusu majeshi yaliyomo ndani ya wizara hiyo ili iweze kufanyiwa marekebisho endapo itabainika kuwa na mapungufu.

Mhandisi Masauni alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, baada ya kumaliza kikao chake na wawawakilishi wakuu na wasaidizi wa vyombo vyote ndani ya wizara hiyo, ambao ni Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji.

Alisema ndani ya Idara ya Uhamiaji, kumekuwepo na watumishi ambao wanachafua taswira na kazi nzuri inayofanywa na jeshi hilo hapa nchini.

Naibu Waziri alisema watendaji hao ni kutoka katika kitengo cha upelelezi, ambao wamekuwa wakishindwa kusimamia vizuri udhibiti wa mipenyo ya mipakani, hivyo kuachia wahamiaji haramu kuingia kupitia mipaka hiyo.

Alisema ipo changamoto ya mipenyo katika mipaka ya Tanzania, kuanzia Kagera, Tanga, Arusha, Katavi na kwingineko, ambayo wakati mwingine imekuwa ikitumika vibaya.

“Mmekuwa mkiona wakati mwingine tunakamata Waethiopia Mbeya, Iringa, haiwezekani watoke kwenye mipaka  waje wakamatiwe huku chini. Tumetoa maelekezo kwa Idara ya Uhamiaji kwamba waandae mkakati kabambe wa kuhakikisha tunadhibiti mipenyo hiyo na bahati nzuri walikuwa wameshaanza,”alisema.

Aliwataka kupitia mpango kazi wao ili waweze kurekebisha kazi ambayo walikuwa wameshaianza na baadaye kuwasilisha serikalini ili iangalie jinsi gani inavyoweza kufanya katika kurekebisha tatizo hilo la uingiaji holela wa wahamiaji haramu katika mipaka.

Masauni alisema wamegundua kuna mapungufu kwa maofisa uhamiaji wa kitengo cha uchunguzi, ambao wana jukumu la kwenda kwenye baadhi ya kampuni na mashirika kufanya msako wa wahamiaji haramu, wanaoharibu kazi nzuri ya jeshi hilo ya kushughulika na wahamiaji haramu.

“Kama tunaona kuna watu ambao hawaendi samabamba na kasi tunayoitaka, ikiwemo wengi waliopo jijini Dar es Salaam, tumeagiza waondoshwe mara moja. Kesho tutaangalia wale ambao tutajiridhisha kwamba hawaendi na kasi yetu waondoke, wakatafutiwe sehemu ambayo wanaweza kufanya kazi, hii ndio awamu tano,”alisema Masauni.

MIKATABA YA MAJESHI

Alisema majeshi yana mikataba mingi kama ule wa Jeshi la Polisi pale Oysterbay na kwamba, wakati umefika wa mikataba yote ambayo majeshi yameingia ihakikiwe na kupitiwa upya.

Masauni alisema lengo ni kuona kama kuna mapungufu yoyote na kama kuna haja ya kufanya mazungumzo na watu wote waliopitia mikataba hiyo, yafanyike haraka ili iweze kwenda sambamba na malengo ya serikali.

Alisema wanataka kuhakikisha kwamba kila watakachokifanya kinakuwa na tija kwa asilimia 100 kwa serikali na wananchi.

AJIRA ZA MAJESHI

Alisema suala la wizara hiyo kusitisha ajira zote za majeshi baada ya kikao hicho na wakati wowote kuanzia sasa, zitatangazwa na wananchi watumia fursa hiyo kuomba nafasi ambazo wana sifa nazo.

“Mtakumbuka katika bunge hili la bajeti linaloendelea, tulisitisha ajira zote ambazo ziko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa lengo la kukaa kama serikali kwa mazungumzo na kuangalia namna ya kuboresha na kuondoa mapungufu ya utaratibu uliokuwa unatumika ili kuboresha," alisema.

Alisema suala la ajira ni mkakati ambao unahitaji muda na umakini wa hali ya juu, hivyo waliona watoe taarifa ili isionekane serikali ina kauli mbili.

Alisema wananchi wasubiri watapata taarifa kupitia vyombo vya habari ili wachangamkie fursa hiyo, ambapo kwa Jeshi la Zimamoto pekee litaajiri  watumishi takribani 522 na kwa Idara ya Uhamiaji wataajiri watu 702.

Alisema wameendelea kuwachukulia hatua na kuwafukuza kazi watumishi, ambao ni askari waliokuwa wakitumia vyeti feki na wale waliokuwa wakitumia vyeti vya kaka, dada ama ndugu zao.

Masauni alisema matumizi ya vyeti vya aina hiyo hivi sasa hayana nafasi katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano yenye kauli mbiu ya hapa kazi tu.

HALI YA USALAMA WA NCHI.

Aliwatoa wasiwasi wananchi na kusema kuwa nchi iko salama na vyombo vyote vya ulinzi vimejipanga vyema na yeyote atakayethubutu kuhatarisha amani, atashughulikiwa  bila woga.

Naibu waziri huyo alisema kazi ya majeshi ni kulinda amani na usalama wa nchi na raia wake, hivyo maisha ya Mtanzania mmoja kupotea kwa serikali ni jambo kubwa na ndio maana Jeshi la Polisi limeendelea kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwabaini wanaojihusisha na mauaji ya raia.

"Kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika ya kudhibiti watu wanaofanya vitendo vya uhalifu na tutaendelea kuwashughulikia ipasavyo," alisema Masauni.

No comments:

Post a Comment