Tuesday, 31 May 2016
MUME ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA DADA WA BILIONEA MSUYA
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inamshikilia mume wa Aneth Msuya, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mkewe yaliyotokea wiki iliyopita, eneo la Kibada, Temeke.
Pia, inamtafuta mfanyakazi wa ndani, ambaye aliondoka siku moja kabla ya mauaji hayo ili kubaini sababu iliyomuondoa nyumbani kwa Aneth.
Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro, alisema jana kuwa, kutokana na mauaji hayo, wameandaa timu ya upelelezi na wataalamu kwa lengo la kubaini waliohusika katika mauaji hayo.
“Tumeandaa timu ya upelelezi na watalaamu kwa ajili ya kuwabaini watu waliojihusisha na mauaji hayo, ambapo hadi sasa tumefanikiwa kumkamata mume wake na jitihada bado zinaendelea kwa ajili ya kumpata dada wa kazi ili kubaini kitu gani kilichomuondoa siku moja kabla ya mauaji,’’ alisema.
Sirro aliwataka wananchi wawape muda wa kufuatilia mauaji hayo kwa lengo la kufahamu tatizo au chanzo chake.
Aneth (30), alikuwa ni mtumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, ambaye aliuawa Mei 25, mwaka huu, kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo, polisi wanawashikilia watu wanne, maarufu kwa jina la Panya Road, wakiwa na marungu na mapanga, baada ya kuvamia nyumbani kwa mfanyabiashara Thomas John.
Alisema watu hao walikamatwa Mei 25, mwaka huu, saa 5.15 asubuhi, maeneo ya Vingunguti Mtakuja, Dar es Salaam.
Watuhumiwa hao ni Stephen Antony (21), Selemani Abdallah (30), Nassoro Anuary (21) na Yussuf Abballah (22) .
Katika tukio lingine, polisi inawashilia watuhumiwa 11 wakiwa na mapanga, visu na marungu, ambao walikamatwa Mei 21, mwaka huu, saa 1.00 usiku, maeneo ya Kivule Nyang’andu.
Watuhumiwa hao ni Lilo Meng’anyi (18), Abas omarty(19), Sambulu Odickson (18), Ayub Mohamed(21), Samwel Milaba(20), Emannulel Nyangi(18), Moses Antony (19), Falijara Salehe(27), Adam Mohamed(23), Ally Said (35) na Sylivester Gideon (22).
Aidha, Sirro alisema wanawashikilia wamiliki sita wa madanguro, wanaouza miili na kaka poa katika maeneo mbalimbali wilayani Temeke.
Wamiliki hao ni Chiku Msafiri, Diula Victor, Ally Mwinyimvua, Helen Newe, Mrisho Khalifan na Zaina Mussa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment