Tuesday, 31 May 2016
DK. SHEIN AWATAKA WANACCM Z'BAR KUENDELEZA USHINDI
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wanachama na wapenzi wa CCM kisiwani Pemba, kuendeleza vuguvugu la ushindi hadi uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.
Dk. Shein amesema vuguvugu hilo halina budi kwenda sambamba na usimamizi makini wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya 2015/2020, ambayo ndio chachu ya ushindi wa CCM katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi, mwaka huu.
Dk. Shein alisema hayo jana, wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya mashina hadi wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Kazi ya chama cha siasa wakati wote ni kuendeleza vuguvugu la kisiasa, ambalo litawaweka wanachama na wapenzi wake pamoja kwa lengo la kuimarisha uhai wake na kujipambanua katika kutekeleza malengo yake kwa jamii,” alisema.
Alisema viongozi hao wana kazi kubwa inayowakabili wana CCM na wananchi, ambayo ni kutekeleza Ilani na kuangalia namna serikali itakavyofanya kazi kwa kutekeleza Ilani hiyo.
Dk. Shein aliwapongeza na kuwashukuru viongozi hao kwa kusimama imara na kwa ujasiri mkubwa hadi CCM ikaibuka na ushindi wa kishindo, kwa mgombea wake wa urais huku ikikomba viti vyote vya uwakilishi na udiwani Unguja na Pemba.
Aliwakumbusha viongozi hao kuwa mwaka ujao, Chama kitafanya uchaguzi wake wa kuwapata viongozi, hivyo hawana budi kuanza kujiandaa.
“Ni uchaguzi utakaoimarisha Chama chetu kwa kupata viongozi makini na wenye uwezo wa kukiongoza na kutuletea ushindi katika uchaguzi wa 2020,” Dk. Shein alisema huku akiwasisitiza viongozi hao kwamba sasa ni kazi tu hakuna kulala.
Katika hatua nyingine, Dk. Shein alisema Chama hakitawavumilia viongozi, ambao hawatatimiza majukumu yao hivyo kuwatanabahisha viongozi katika Chama kuepuka ubabaishaji.
Dk. Shein yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya siku tatu, kuwashukuru wanachama na wapenzi wa chama hicho kwa ushindi mkubwa walioupata katika uchaguzi mkuu uliopita.
Katika hatua nyingine, wanachama wa CCM kisiwani Pemba, wamesema ushindi wa Chama katika uchaguzi uliopita unatokana na umoja na ushirikiano kati yao na viongozi wa Chama, sambamba na ukomavu wa kisiasa alionao Dk. Shein.
Viongozi hao walitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Dk. Shein kwa ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu uliopita na kusisitiza kwamba, ushindi huo utaendelezwa mpaka katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020, kwani wanaamini kuwa hakuna tena uchaguzi katika kipindi hicho.
Katika maelezo yao, viongozi hao walisema ukomavu wa kisiasa alianao Dk. Shein, ndio chachu ya mafanikio ndani ya Chama na ushindi wake katika uchaguzi wote.
Aidha, viongozi hao walimueleza Dk. Shein kuwa yeye ndiye Rais halali wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliyechaguliwa na wananchi kwa kura nyingi, hivyo wataendelea kumuunga mkono katika kuhakikisha Zanzibar inaendelea kupata maendeleo endelevu.
Pamoja na hayo, viongozi hao walitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuunda serikali makini na kusema wana imani na viongozi aliowateua kushirikiana naye ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi hao walitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais Dk. John Magufuli kwa ushindi wake mkubwa pamoja na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment