Tuesday, 31 May 2016

VURUGU BUNGENI, LISSU, BULAYA, MDEE, ZITO, LEMA WAPIGWA STOP KUHUDHURIA VIKAO

MALUMBANO na vurugu zimelitikisa bunge na kumlazimu Naibu Spika, Dk. Tulia Akson, kuamuru askari wa bunge kuwatoa wabunge waliokuwa wakifanya vurugu huku wengine wa kambi ya upinzani wakisusia kuendelea na kikao.

Vurugu hizo zilijitokeza baada ya Naibu Spika kutokubali kujadiliwa kwa hoja kuhusu sakata la kurejeshwa nyumbani wanafunzi 7,802 wa Stashahada ya Mafunzo ya Ualimu wa Sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma.

Ili kunusuru hali ya hewa isichafuke zaidi, Dk. Akson aliamua kusitisha shughuli za bunge hadi saa kumi jioni na kuagiza Kamati ya Uongozi ya Bunge ikutane ili kujadili suala hilo.

Baada ya bunge kurejea jioni, Naibu Spika alisema halitaweza kujadili hoja hiyo hadi serikali itakapowasilisha taarifa rasmi bungeni kama ilivyoafikiwa na kamati ya uongozi, hivyo alimuagiza Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Issac Kamwele, kuendelea kuhitimisha hoja ya wizara yake kuhusiana na mapato na matumzi ya wizara hiyo.

Uamuzi huo haukukubaliwa na wabunge wa kambi ya upinzani, ambao walianza kufanya vurugu kwa kugonga meza huku mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika, akitolewa nje na askari wa bunge kutokana na kitendo chake cha kukaidi amri ya spika ya kuacha kufanya fujo.

Baada ya wabunge hao wa upinzani kuendelea na vurugu bungeni, aliamuru askari wa bunge kuwatoa wabunge wote wa kambi hiyo ili shughuli zilizopangwa ziendelee.

Baada ya kujadiliana na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wabunge wa kambi hiyo walilazimika kuondoka huku wakiwarushia vitabu na makaratasi askari wa bunge.

Kutokana na vitendo hivyo vilivyoonyeshwa na wabunge wa upinzani, Dk. Tulia aliagiza kufikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.

Awali, baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu, Naibu Spika, alitoa nafasi kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, kutoa kauli ya serikali kuhusiana na kurejeshwa nyumbani kwa wanafunzi hao.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Profesa Ndalichako aliliambia bunge kuwa, serikali ililazimika kuwarejesha nyumbani wanafunzi hao kutokana na mgomo wa walimu waliokuwa wakifundisha kozi hiyo.

Waziri huyo alieleza kuwa mgomo huo wa walimu umedumu kwa kipindi cha mwezi mmoja, ambapo katika kipindi hicho, wanafunzi hao hawakuwa wakiendelea na masomo.

Alisema licha ya kuweko kwa madai ya walimu hao, taarifa ya mkaguzi wa ndani chuoni hapo, ilionyesha kupingana na baadhi ya madai hayo.

“Serikali tuliona ni busara kuwarudisha nyumbani wanafunzi hao, wakati tukiendelea na ufumbuzi wa jambo hilo, licha ya kuwa wanafunzi hao hawana makosa kwa kuwa wenye makosa ni walimu,” alisema Ndalichako.

Aliongeza kuwa serikali ilifanya mazungumzo na walimu hao kwa kipindi chote hicho bila kupata muafaka na ndiyo maana imeamua kufikia uamuzi huo.

Baada ya Profesa Ndalichako kutoa taarifa hiyo,  Juma Nkamia (Chemba - CCM), aliomba muongozo wa kiti kuhusiana na sakata hilo, akihoji ni kwanini serikali haikuona umuhimu wa kuumaliza mgogoro huo na walimu, badala yake imewaondoa wanafunzi hao chuoni.

Pia, Nkamia alitoa hoja ya kutaka kuahirishwa kwa shughuli za bunge zilizopaswa kuendelea, badala yake lijadili hoja hiyo kwa kuwa ni muhimu na yenye maslahi.

Dk. Tulia alisema kwa kuwa serikali imeshatolea taarifa kuhusiana na jambo hilo, ni dhahiri kwamba inalifahamu vyema na inalifuatilia kwa karibu.

Alibainisha kwamba serikali imetoa maelezo kuwa katika mwezi huu, ilikuwa inajaribu kuona namna inavyoweza kutatua suala hilo kwa kufanya mazungumzo na walimu wenye madai, lakini inaonekana mazungumzo yao hayajafikia muafaka.

Naibu Spika alisema bunge haliwezi kuanza kuuliza maswali kwa vitu ambavyo hawakuletewa, kwani taarifa ya mkaguzi wa ndani ambayo serikali imeizungumzia kwenye taarifa yake bunge, hajaipata.

“Kwa sababu hoja ya Nkamia ilikuwa kwenye muongozo, kwa hiyo muongozo wangu ni kwamba, serikali imeshatoa maelezo juu ya suala hilo, kama kuna jambo ambalo hatujaelewa katika maelezo ya waziri, hilo ndilo linaweza likaulizwa,” alisema.

Baada ya hoja hiyo kugonga mwamba, Joshua Nassari (Arumeru Mashariki - CHADEMA),  aliomba muongozo wa spika kutoa hoja kama iliyowasilishwa na Nkamia.

Nassari alisema kwa mujibu wa kanuni ya 68 (7) na 69, aliiomba mjadala uliokuwa ukiendelea kama ilivyopangwa kwenye 'order paper' usitishwe, badala yake bunge lijadili suala la wanafunzi wa UDOM.

Aliongeza kuwa wanafunzi hao juzi, walilazimishwa kuondoka kwenye maeneo ya chuo kwa saa 24, hali iliyosababisha kuzagaa hususan nyakati za usiku.

Baada ya kutolewa kwa hoja hiyo, malumbano na vurugu ziliibuka kwa baadhi ya wabunge, wakiwataka wenzao ambao hawakuinuka kuiunga mkono hoja hiyo kwa kuwataka kuinuka.

Hali hiyo ilimlazimu Naibu Spika kuwatuliza wabunge hao ili aweze kuitolea muongozo hoja hiyo.

Akijibu muongozo wa Nassari, Dk. Tulia alisema mbunge atalazimika kutoa sababu ni kwanini anataka mjadala huo uahirishwe, kama ambavyo kanuni 69, kanuni ndogo ya pili inavyoeleza.

“Spika atakuwa na maoni kwamba, kuahirishwa kwa hoja hiyo ni kinyume cha uendeshaji bora wa shughuli za bunge, hivyo atakuwa na mamlaka ya kukataa kuitoa hoja hiyo iamuliwe, vinginevyo papo hapo atawahoji wabunge juu ya hoja hiyo kadri atakavyoona inafaa,” alisema Dk. Tulia.

Hivyo kwa mujibu wa kanuni ya 69, fasiri ya pili, ambapo yeye kama spika kwa muda huo hakuona hiyo hoja kama ni bora katika uendeshaji bora wa bunge na akitumia kanuni ya 47 kwa kutumia fasiri 4, hakuridhika kwamba jambo hilo ni la dharura.

Uamuzi huo wa kiti uliibua muendelezo wa vurugu na kelele kwa wabunge kukataa kukubaliana nao.

Licha ya Dk. Tulia kuwasihi mara kadhaa wabunge wa kambi ya upinzani watulie na kuacha kelele ili shughuli zingine ziendelee, wabunge hao walikaidi.

Agizo hilo la Naibu Spika kwa wabunge wa upinzani, halikuzaa matunda, hali iliyomlazimu kuagiza askari wa bunge kuingia ndani kuwatoa nje wabunge waliokuwa wakipiga kelele.

Baada ya askari wa bunge kuingia ndani na kuanza kuwatoa nje wabunge, Dk. Tulia aliahirisha shughuli za bunge mpaka saa 10  jioni.

Wanafunzi hao wa UDOM, walikuwa wakisoma kozi maalumu ya sayansi, iliyoanzishwa chuoni hapo ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi kwenye shule za sekondari.

Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, polisi walilazimika kuweka ulinzi mkali kwenye maeneo yanayozunguka viwanja vya bunge kwa kile kilichoelezwa kuwa, wanafunzi hao walikuwa wakitaka kuandamana.

Juzi, baadhi ya mawaziri na wabunge waliofika chuoni hapo kwenye maadhimisho ya siku ya usafi ya kila mwezi, waliwahakikishia kuwa serikali inaendelea kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo uliopo kati ya walimu na serikali.



Wakati huo huo, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, imetoa onyo kali kwa wabunge saba wa kambi ya upinzani, waliohusika kufanya vitendo vya vurugu na kudharau mamlaka ya Spika, Januari 27, mwaka huu.

Wabunge hao waliopewa onyo kali ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Gobless Lema (Arusha Mjini), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Halima Mdee (Kawe, John Heche (Tarime Vijiji),  Pauline Gekul (Viti Maalumu) na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini).

Akisoma maamuzi hayo ya kamati, Mwenyekiti wa kamati hiyo, George Mkuchika, alisema maamuzi hayo yamefikiwa kwa kuzingatia sheria mama ya maadili na madaraka ya Bunge pamoja na kanuni zake.

Mkuchika alisema wabunge waliohusika kufanya makosa hayo pindi wakirudia tena, wataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge.

"Vitendo hivi ni vya utovu wa nidhamu, ikiwemo Lema kuvua koti na tai bungeni, akiashiria utayari wa kupigana na spika, hakipaswi kufanywa na kiongozi,"alisema Mkuchika.

Mkuchika alisema kamati hiyo pia imebaini muongozo wa spika kutumika vibaya, hivyo imeliomba bunge kuangalia upya utaratibu wa kuomba miongozo.

Katika hatua nyingine, kamati hiyo ilitoa maazimio kwa wabunge Ester na Lissu, kutohudhuria vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge la 11 kuanzia jana, pamoja na vikao vyote vya mkutano wa nne wa bunge  hilo.

Pia, wabunge Pauline, Lema na Zitto hawaruhusiwi kuhudhuria vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge la 11 kuanzia jana, ambapo Heche hataruhusiwa kuhudhuria vikao 10 mfululizo vya mkutano wa tatu wa bunge hilo.

Wakichangia baada ya kutolewa kwa maazimio hayo, mbunge Ridhiwan Kikwete (Chalinze-CCM), alisema adhabu hiyo ni sahihi na inapaswa kuchukuliwa kwa wabunge wasiokuwa na nidhamu.

Naye Joseph Msukuma (Geita Vijijini- CCM), alisema lazima hatua kali zichukuliwe kwa wabunge hao ili  wengine wajifunze.

No comments:

Post a Comment