Thursday, 26 May 2016

UHUSIANO WA TANZANIA, OMAN KUIMARIKA-SAMIA


MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itaendelea kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Oman katika nyanja mbalimbali kwa faida ya nchi zote mbili.

Samia aliyasema hayo jana, alipokutana na Balozi wa Oman hapa nchini anayemaliza muda wake, Saud Ali Mohamed Al-ruqaishi, ambaye alikwenda ofisini kwake Ikulu kwa ajili ya kuaga.

"Tanzania tunajua tuna wajibu wa kukuza uhusiano na Oman, uhusiano wetu si wa kibalozi tu bali umeota mizizi kwa kuwa ni wa muda mrefu na wa kindugu,"alisema.

Alibainisha kuwa serikali imekuwa na uhusiano na Oman katika nyanja za elimu na hasa elimu ya juu, ambapo nchi hiyo imesaidia ujenzi wa Chuo cha Afya Mbweni na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Kwa mujibu wa Samia, serikali ya Oman imeanzisha Mfuko Maalum ikiwa ni sehemu ya ufadhili kwa wanafunzi wa Zanzibar katika elimu ya juu pamoja na kukijengea uwezo SUZA.

Makamu wa Rais aliiomba Oman kuangalia uwezekano wa uwekezaji katika sekta za kilimo na biashara ambako kuna fursa nyingi za uwekezaji.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Al-ruqaishi aliishukuru Tanzania kutokana na ushirikiano aliopewa muda wote alipokuwepo nchini, jambo ambalo limwemwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment