Thursday, 26 May 2016
KAMPUNI 52 ZA UMEME ZATAKA KUWEKEZA NCHINI
Na Mwandishi Maalum, Lusaka
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, amesema hadi sasa serikali imekwishapokea maombi 52 kutoka kwa kampuni mbalimbali ambazo zinataka kuwekeza kwenye sekta ya umeme Tanzania.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi jioni, wakati akizungumza na Watanzania waishio Zambia katika mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka.
“Haya maombi yamekwishapokelewa na wenye kampuni wamekwishahojiwa kuangalia uwezo walionao katika suala zima la uwekezaji wanaotaka kuufanya na tukiwapata wenye uwezo na wenye nia ya dhati watapatiwa miradi ya kuiendesha,” alisema.
Aliwataka Watanzania hao waishio Zambia watumie fursa ya uwepo wao huko kutafuta marafiki ambao wanaweza kuja kuwekeza kwenye miradi nchini, kwani serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu wakati wananchi wanahitaji kupatiwa huduma muhimu.
“Serikali peke yake haiwezi kufanya kazi ya uwekezaji, kwa hiyo tunahitaji kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo na ndiyo maana kule kwenye mkutano nimewaeleza washiriki kwamba milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi," alisema.
Alisema kupatikana kwa umeme wa uhakika kutawezesha wananchi wengi zaidi kujiingiza katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuinua uchumi wa nchi na maendeleo ya taifa.
Alisema malengo ya serikali ni kuona kuwa nchi inakuwa na mitambo mingi ya kuzalisha umeme na umeme wote unaozalishwa na mitambo hiyo inaunganishwa na gridi ya taifa ili kuondokana na tatizo la mgawo wa umeme nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati, vikiwemo gesi asilia, makaa ya mawe, madini ya urani, maji, upepo, nishati ya joto kutoka ardhini na nishati inayotokana na vinyesi vya mifugo ambayo alisema vinatumika kwa watu wachache.
Alisema kupatikana kwa gesi asilia nchini kumeleta neema, ambapo mabomba ya gesi yamekwisha jengwa kutoka Mtwara hadi Kinyerezi na kutoka Kilwa-Songosongo hadi Dar es Salaam.
“Sasa hivi kuna utafiti unaendelea juu ya uwezekano wa kusambaza gesi ya kupikia nyumbani. Tumeanza pale Mikocheni na sasa hivi wanafanya utafiti mwingine kule Mtwara ili wananchi watumie gesi hii kupikia badala ya mkaa,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment